Katibu Msaidizi wa Idara ya Mabinti na Uwezeshaji ya Taasisi ya Mama Asemewe, Beatrice Mwahegili, amewataka vijana hususan mabinti nchini kuheshimu, kulinda na kutunza amani ya Tanzania, akisisitiza kuwa hakuna Tanzania nyingine ya kukimbilia endapo amani iliyopo itapotea.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo, Alhamisi Desemba 4, 2025, Beatrice amesema vijana wanapaswa kuamka na kutokubali kutumika kwa maslahi ya watu wachache, sambamba na kuwakataa wanaohamasisha vitendo vyovyote vinavyoweza kuvuruga amani ya nchi.
“Tunapinga vikali maandamano yanayoendelea kuhamasishwa tarehe 09. Tarehe hiyo ni siku muhimu kwa Taifa letu kwani ndiyo siku tulipopata uhuru—si siku ya vurugu au kuhamasisha machafuko. Tanzania tumeikuta ikiwa na amani, na kama vijana, wajibu wetu wa kwanza ni kuitunza. Hatuna Tanzania nyingine, na tukiharibu hii, hatuna sehemu ya kukimbilia,” amesema.
Beatrice amebainisha kuwa amani iliyopo nchini imekuwa chachu ya maendeleo na ustawi wa mabinti, vijana na jamii kwa ujumla, huku ikichangia upatikanaji wa fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
“Kipindi cha Rais Samia kimetugusa kwa kiwango kikubwa sana, hasa sisi mabinti. Kupitia mikopo ya elimu ya juu, mabinti wengi kutoka familia duni wamepata nafasi ya kusoma na kuepuka vishawishi mbalimbali. Rais Samia pia amepanua wigo wa elimu kwa wanaopata ujauzito wakiwa shuleni, na zaidi ametupa Wizara ya Vijana inayobeba maslahi yetu,” amesisitiza.
Beatrice amewataka mabinti na vijana kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kulinda utulivu wa nchi, akisema maendeleo yanayoonekana leo hayawezi kudumu bila kuwepo kwa amani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED