Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla, amesema kupumzika kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu, kwao ni mserereko na watashinda kwa kishindo.
Akizungumza katika Kata ya Ruaha, wilayani Kilosa, jimbo la Mikumi, mkoani Morogoro, akiendelea na ziara yake ya siku saba mkoani humo, amewashukuru wananchi kwa mapokezi na kwa namna walivyokipa ushindi CCM Uchaguzi Serikali za Mitaa, 2024.
“Zamani tuliwahi kuonjeshwa sumu, kweli si kweli, na waliotuonjesha sumu safari hii wamepumzika nani hao, CHADEMA, kwetu ni mserereko.Tuhakikishe daftari likipita awamu ya pili tujiandikishe vizuri na sisi wote tutakwenda kukipa ushindi Chama Cha Mapinduzi,” alisema.
Makalla alisema alipokwenda hapo mwaka jana kufunga kampeni za Serikali za Mitaa aliwapa salamu za CCM kwamba, wakichague, hivyo amerudi kuwashukuru.
“Niliwaomba mtuchague nikawaambia yajayo yanafurahisha.Na haya yote tunayotamba nayo ni kazi nzuri ya Mwenyekiti wetu na Rais Samia Suluhu Hassan, kama msemaji ninatamba kwa sababu Rais Samia ametoa fedha nyingi kuliko awamu yoyote,” alisema.
Aliwahaahidi kwamba CCM kitaendelea kuwa pamoja na wananchi, huku akiwaeleza kuwa kama walivyokuwa nacho wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa vivyo hivyo wakiunge mkono katika uchaguzi ujao na kupata kura za kishindo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED