Makalla: Wabadhirifu fedha ujenzi hospitali Ifakara kushughulikiwa

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 01:20 PM May 09 2025
Katibu  wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla.
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla.

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla, amesema Hospitali ya Halmashauri ya Mji Ifakara, Kilombero, inayojengwa eneo la Kiberege, mkoani Morogoro, yenye hadhi ya wilaya haijakamilika kutokana na ubadhirifu wa fedha.

Amewaeleza wananchi wilayani humo kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, atakwenda hapo kulifanyia kazi suala hilo ili ikamilike na waliohusika kushughulikiwa.

Ameyasema hayo Mei 8, 2025,  katika mkutano wa hadhara uliofanyika Ifakara, wilayani Kilombero, mkoani humo,nikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya siku saba.

Akizungumzia kuhusu changamoto za miradi ya barabara, Makalla alisema amezungumza na Waziri wa Ujenzi ambaye amemhakikishia ujenzi utaendelea.

Vilevile, alisema amezungumza pia na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amemhakikishia baada ya bajeti atakwenda huko kushughulikia.

“Nimepokea changamoto ya stakabadhi ghalani kwanza mfumo huu ni mzuri nimetoka Lindi na Mtwara wamefaidika, kwa Kilombero kwa halmashauri zenu zote mbili vituo ni vichache na fedha zinachelewa..Mkuu wa Mkoa umesikia tuongeze vituo na fedha zilipwe kwa wakati.

“Hatukimbii changamoto tunakabiliana nazo hakuna chama mbadala. Changamoto mlizonazo haziwezi kumalizwa na hao wasiokuwa na dhamana,” alisema.