Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, linamshikilia Marry Timotheo, mkazi wa Garijembe kwa tuhuma za kumuua mtoto wake Scola Mwaba (10) , mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Ngonde.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amethibitisha tukio hilo na kueleza kuwa limetokea Decemba 9,2025 majira ya saa 6:30 mchana eneo la Garijembe mtuhumiwa amuadhibu mtoto wake kwa kumpiga kichwani na kitu kizito akimtuhumu kuwa ni mtukutu.
“Taarifa za awali za uchunguzi zinaeleza kuwa chanzo cha tukio ni kujichukulia sheria mkononi ambapo baada ya kumpiga hadi kufariki dunia, Marry alimtupa mwanae shambani jirani na nyumba yake kwa msaada wa jirani yake Sharifa Nzalanje , ambaye naye anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kushiriki kuficha kosa,” amesema Kuzaga.
Kamanda Kuzaga amesema upelelezi wa kesi hiyo unakamilishwa kabla ya kuwafikisha watuhumiwa katika hatua zinazofuata za kisheria.
Ametoa wito kwa wazazi au walezi kuepuka vitendo vya kujichukulia sheria mkononi kwa kutoa adhabu kali kwa watoto na badala yake kutumia mbinu za malezi na maadili zitakazosaidia kuwalea bila kusababisha madhara kama vile vifo au ulemavu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED