Mama wa kambo aangua kilio baada ya kuhukumiwa kifungo

By Joctan Ngelly , Nipashe
Published at 01:52 PM Jun 11 2025
Mama wa kambo aangua kilio baada ya kuhukumiwa kifungo.
Picha: Joctan Ngelly
Mama wa kambo aangua kilio baada ya kuhukumiwa kifungo.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Geita imemhukumu mkazi wa Nyatorotoro, Janeth Emmanueli (20) kutumikia kifungo cha miaka mitano gerezani kwa kosa la kumchoma na maji ya moto kwenye makalio mtoto mvulana mwenye umri wa miaka mitatu na kumsababishia maumivu makali.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Buruno Bongole baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha kosa hilo pasipo kuacha shaka yoyote.

Hakimu Bongole alisema mahakama hiyo inatoa adhabu dhidi ya mshtakiwa huyo ili iwe fundisho kwake na kwa wanawake wengine wenye tabia ya kuwachoma na maji ya moto watoto wa kambo kama yake.

Alisema upande wa mshtaka ulikuwa ukiongozwa na Wakili wa Serikali Concessa Desideri ambaya alipeleka mahakamani mashahidi wanne na vielelezo vitatu ambavyo vilithibitisha mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo.

Hakimu Bongole alisema mtoto huyo alikuwa anaishi na mama wa kambo, Janeth, ambaye ni mshtakiwa katika maeneo ya Nyatorotoro wilaya ya Geita. Mshtakiwa huyo alikuwa anamtenda mtoto huyo vitendo vya kikatili mara kwa mara.

Alisema kuwa siku ya tukio hilo Agosti 18, 2024, huko Nyatorotoro wilayani Geita, mshtakiwa huyo alichemsha maji ya moto kisha kumchukua mtoto huyo na kumkaliza kwenye maji ya moto ndipo mtoto huyo aliungua makalio na kupata majeraha na maumivu makali.

Alisema kuwa baada ya tukio hilo, mwenye nyumba alikokuwa anaishi mshtakiwa huyo, alipiga simu Kituo cha Polisi Geita na askari walifika na kumchukua mtoto huyo kisha kumpatia Fomu Na. 3 ya Polisi (PF3) na kupelekwa Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa matibabu. Mtoto alilazwa huko kwa siku tatu. Daktari aliyemfanyia uchunguzi alibaini kuwa mtoto huyo alikuwa anafanyiwa ukatili mkubwa, maana mwili mzima wa mtoto huyo ulikuwa na makovu ya kufinywa na makovu ya kupigwa kwa fimbo.

1

Hakimu Bongole alisema kuwa baada ya mtoto huyo kuruhusiwa kutoka hospitalini, alipelekwa kituo cha kulelea watoto waliofanyiwa ukatili cha Moyo wa Huruma cha Kanisa Katoliki.

Alisema mshtakiwa huyo alikamatwa na alipohojiwa kuhusiana na kosa hilo, alikiri kuhusika. Upelelezi wa kesi hiyo ulipokamilika, alifikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

Wakati hukumu hiyo inasomwa, waliokuwa mahakamani ni pamoja na Mlezi wa Kituo cha Moyo wa Huruma, Susana Viatory, bibi wa mtoto aliyefanyiwa ukatili, Mariam Juma, baba mzazi wa mtoto aliyefanyiwa ukatili, Izack Jeremia, Ofisa Ustawi wa Jamii, Michael Maregesi na mama wa mshtakiwa, Rosemary Protas.

Hakimu Bongole alisema ameangalia ushahidi wa pande zote na kubaini upande wa mashtaka umethibitisha kasa hilo pasipo kuacha shaka yoyote, hivyo mahakama inamtia hatiani mshtakiwa kwa kosa aliloshtakiwa nalo.

Kabla ya kutoa hukumu, hakimu alimpa mshtakiwa nafasi ya kutoa maombolezo ya kupunguziwa adhabu.

Mshtakiwa huyo aliangua kilio na kusema anaomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa ana mtoto mdogo anayemtegemea.

Upande wa mashtaka, ukiongozwa na Wakili wa Serikali Desideri uliomba mahakama itoe adhabu kwa mujibu wa sheria ili kupunguza ukatili wa watoto katika mkoa wa Geita.

Hakimu Bongole alitupilia mbali utetezi wa mshtakiwa na kusema kitendo alichokifanya ni cha kikatili.

Alisema kuchemsha maji ya moto kisha kumchukua mtoto wa mumewe na kumkaliza kwenye maji ya moto ni ukatili uliopitiliza.

"Hivyo mahakama hii inakuhukumu mshtakiwa kutumikia kifungo cha miaka mitano jela au kulipa faini ya Sh. milioni moja pamoja na kulipa mtoto wa mume wako uliyemfanyia ukatili Sh. milioni moja na laki tano. Ukimaliza kifungo chako utakuwa raia mwema kwa jamii," alisema.

Baada ya mshtakiwa huyo kusomewa hukumu yake, aliangua kilio kisha kuanguka chini na kuzimia kwa muda wa takribani nusu saa na alipoamka aliendelea kuangua kilio mahakamani ndipo askari polisi wa kike walimchukua na kumpeleka mahabusu ya mahakama hiyo.

Baadaye Hakimu Bongole alisema mshtakiwa ameshindwa kulipa faini ya Sh. milioni moja pamoja na fidia kwa mtoto aliyemfanyia ukatili, hivyo atatumikia kifungo cha miaka mitano gerezani na akimaliza kifungo chake, lazima amlipe huyo mtoto wa mume wake aliyemfanyia ukatili Sh. milioni moja na laki tano.

2