Matiko ataka udhibiti wa pombe kali kwenye maduka ya vyakula

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 07:36 PM Jun 03 2025
Matiko ataka udhibiti wa pombe  kali kwenye maduka ya vyakula
Picha: Mtandao
Matiko ataka udhibiti wa pombe kali kwenye maduka ya vyakula

Mbunge wa Viti Maalum, Esther Matiko, ameishauri Serikali kudhibiti kwa haraka uuzwaji holela wa pombe kali, ambazo sasa zinapatikana hadi kwenye maduka ya vyakula, akisema hali hiyo ni janga la kitaifa linaloathiri afya na maisha ya vijana wengi.

Akichangia leo Juni 3, 2025, bungeni jijini Dodoma katika mjadala wa makadirio ya bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Matiko amesema matumizi ya pombe hizo — nyingi zikiwa feki — yanasababisha madhara makubwa ya kiafya, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa wagonjwa wa figo.

“Taifa letu linateketea kwa pombe. Vijana wanateketea kwa pombe kali ambazo zingine ni feki. Nilishazitaja, leo sizitaji. Zinauzwa hadi kwenye maduka ya chakula. Mnasema figo ni gharama — kama hatutazizuia, tutatumia fedha nyingi kuwatibu Watanzania hawa,” amesema Matiko kwa msisitizo.

Ameonya kuwa kama hali hiyo haitadhibitiwa mapema, itazidisha mzigo wa matibabu kwa serikali hasa baada ya utekelezaji wa Sheria ya Huduma ya Bima ya Afya kwa Wote kuanza.

Mbunge huyo pia ameitaka Wizara ya Afya kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara kuhakikisha pombe hizo hazisambazwi kiholela mitaani, na kwamba hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wauzaji wasiofuata taratibu.

“Mnatumia mitutu ya bunduki kulinda mipaka ya nchi wakati ndani ya nchi vijana wanaendelea kuteketea. Wengine wanakufa kwa kunywa pombe hizi kali. Mtaani watu wanakufa tu — bodaboda tunawazika kila mara. Taifa linateketea. Hakikisheni mnadhibiti hali hii na wanaouza kiholela ikibidi wakamatwe,” amesisitiza Matiko.