Robo fainali ya mashindano ya wazi ya Taifa ya mchezo wa ngumi inaendelea kwa kasi kwenye viwanja vya Manyara, Tandale jijini Dar es Salaam, ambapo mabondia chipukizi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi wanachuana kuwania nafasi ya kuingia nusu fainali.
Akizungumza kuhusu maendeleo ya mashindano hayo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), Makore Mashaga, amesema jumla ya mabondia 62 wamefanikiwa kufuzu kuingia hatua ya robo fainali.
"Mashindano haya yalianza jana, na hadi sasa tumepata mabondia 62 walioingia hatua ya robo fainali. Tunatarajia kucheza michezo 31, ambapo nusu fainali itapigwa kesho hapa hapa Manyara," amesema Mashaga.
Ameongeza kuwa mashindano hayo si tu ya kuibua vipaji, bali pia ni fursa kwa mabondia kuonyesha uwezo wao ili kupata nafasi ya kuunda kikosi cha timu ya Taifa kitakachojiandaa na mashindano ya kimataifa yanayokuja.
"Tangu mashindano haya yaanze, nimeona vipaji vingi sana kutoka kwa vijana, jambo ambalo limenivutia sana. Tuna matumaini makubwa kwamba tutapata mabondia wa kuaminika kwa ajili ya kuiwakilisha nchi," ameongeza.
Aidha, Mashaga ametoa wito kwa vijana na wadau wa michezo kujitokeza kwa wingi viwanjani kushuhudia mapambano na kuunga mkono jitihada za kuinua mchezo wa ngumi nchini.
"Mabondia wetu chipukizi wanaonyesha viwango vya hali ya juu, tunahitaji sapoti ya jamii ili tuwatie moyo na kukuza mchezo huu," amesema.
Mashindano hayo ni sehemu ya kalenda ya BFT katika kuendeleza mchezo wa ngumi za ridhaa na kuchagua vipaji kwa ajili ya mashindano ya kikanda na kimataifa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED