Mwakilishi Jimbo la Ole atoa mipira ya maji, aahidi kutoa mifuko 100 ya saruji

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:46 AM Dec 11 2025
Mwakilishi Jimbo la Ole atoa mipira ya maji, aahidi kutoa mifuko 100 ya saruji
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Mwakilishi Jimbo la Ole atoa mipira ya maji, aahidi kutoa mifuko 100 ya saruji

Katika jitihada za kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu, Mwakilishi wa Jimbo la Ole, Seif Hamad ametoa mipira mipya ya maji kwa kijiji cha Simaongwe, vifaa ambavyo vitasaidia kuongeza mtiririko wa maji safi na kupunguza adha ya wananchi waliyoipata baada ya ujenzi wa barabara kuharibu miundombinu na mfumo mzima wa upatikanaji wa maji.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Mwakilishi huyo alisema kuwa kipaumbele chake ni kuona changamoto za maji zinamalizika hatua kwa hatua, na kwamba Serikali ya Jimbo la Ole inaendelea kushirikiana na wananchi kuhakikisha huduma za msingi zinawafikia wote tena kwa wakati. 
Katika hatua nyingine,  Mwakilishi huyo ametembelea eneo la ujenzi wa daraja linaloendelea kujengwa katika eneo la kwa Pweza linalounganisha Shehia ya Ng'ambwa, Shehia ya Mchangamrima na Ole, mradi muhimu unaotarajiwa kuunganisha maeneo ya kilimo na Makazi ya Wananchi. 

1


Wakati wa ziara hiyo, ameahidi kuchangia mifuko ya saruji 100 ili kuongeza kasi ya ujenzi na kuhakikisha daraja hilo linakamilika kwa wakati. Wananchi wa eneo hilo wamesema kukamilika kwa daraja hilo kutakuwa mkombozi mkubwa kwao, kwani litapunguza adha za mvua, kurahisisha usafiri wa wanafunzi na kufungua njia za kiuchumi kwa wakulima na wafanyabiashara.

Amesisitiza kuwa ataendelea kufanya kazi kwa karibu na wananchi na viongozi wa shehia kuhakikisha kila ahadi inaleta matokeo chanya, akisema: “Uongozi ni huduma, na ninataka wananchi wa Ole waone matunda ya imani yao". amesema