Mwandishi wa habari amrithi Jokate UWT

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 12:00 PM May 20 2024
Suzan Kunambi.
Picha: Maktaba
Suzan Kunambi.

KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imemteua Mwandishi wa Habari, Suzan Kunambi, kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT), ambaye amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Magharibi A, visiwani Zanzibar.

Suzan ameteuliwa kuongoza nafasi hiyo baada ya aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo, Jokate Mwegelo kuteuliwa kwenda kuongoza kwenye Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM) katika nafasi ya Katibu Mkuu.

Kamati hiyo ya Halmashauri Kuu ya CCM, katika kikao chake maalum kilichofanyika Ofisi Kuu ya chama hicho, Kisiwandui, Zanzibar chini ya Makamu Mwenyekiti wake na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, pamoja na mambo mengine, ilimteua Khamis Yusuf Mussa (Pele), kuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho Jimbo la Kwahani, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.

‘Pele’ atapeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mdogo wa ubunge unaotarajiwa kufanyika Juni 8, mwaka huu kutokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Ahmada Yahya Shaa, aliyefariki Aprili 8, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Amos Makalla, Kamati Kuu hiyo ilizipongeza serikali zote mbili kwa namna zinavyoendelea kuwatumikia wananchi kwa vitendo kupitia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho ya mwaka 2020-2025.

MNEC AKABIDHI LESENI WANAWAKE

Wakati huo huo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) Mkoa wa Simiyu, Gungu Silanga, amekabidhi leseni kwa wachimbaji wa madini wanawake wa mkoa huo, kwa ajili ya kuwarahisishia kazi zao.

Silanga ameyasema hayo mbele ya Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, wakati akikabidhi leseni kwa wachimbaji hao wanawake.

"Mimi ni MNEC wa Simiyu waliponifuata nikawaambia sawa lakini nendeni mkaunde kikundi kitakachokuwa na wawakilishi wa wilaya zote tano za mkoa huu. Kinamama hawa ni wasikivu walifanya hivyo.”

Silanga amefafanua kuwa baada ya kukamilisha taratibu hizo aliwasiliana na ofisa madini aliyempa fomu na kuwakabidhi leseni Jumamosi.

Waziri Mavunde amemshukuru Silanga kwa moyo wake wa uelewa na kufuata maelekezo ya serikali na kwa hatua hiyo amewapa heshima kinamama wa Mkoa wa Simiyu.

"Umepandikiza mbegu kubwa sana, ulichokifanya kwa kinamama hawa kina maana kubwa katika uchumi, umekuwa muungwana, mstaarabu na msikivu kwa kuwajali wanawake wa Simiyu.

"Uchimbaji ni gharama kubwa sana, serikali inaangalia mipango mizuri ya kusaidia na kuwezesha kinamama na vijana kufanya uchimbaji na wizara itakusaidia MNEC," amesema Mavunde.