Mwenge kukagua miradi saba yenye thamani ya bil.44.5 Ilala

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 08:45 PM Jun 03 2025
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo.

Mwenge wa Uhuru Wilaya ya Ilala unatarajiwa kukagua miradi saba ya maendeleo Wilayani humo yenye jumla ya Sh.Bilion 44.5 utakaotembea kilomita 82.6.

Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo mara baada ya kukabidhiwa mwenge huo katika Viwanja vya Mnazi Mmoja  ukitokea Wilaya ya Kigamboni.

Miradi itakayokaguliwa katika mbio hizo za Kitaifa 2025 ni uzinduzi mradi wa nishati safi Soko la Kimataifa la samaki Feri, Kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa barabara ya Magengeni-Chang’ombe -African School-Sanene Tabata.

Mradi wa kiwanda kidogo cha kutengeneza samani unaotekelezwa na kikundi cha vijana kiitwacho ULIPO TUPO kinachojishughulisha na uchongaji wa madawati kilichopo Tabata.

Pia utakagua na kuweka jiwe la msingi ujenzi wa mradi wa usambazaji wa maji kusini mwa Dar es Salaam uliopo Pugu Stesheni. 

Utakagua na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa kituo cha afya cha Mzinga kilichopo Kata ya Mzinga utakaogharibu kiasi cha Sh.Bil.4 na uzinduzi katika mradi wa ujenzi wa kituo cha polisi -Kivule.

Pamoja na  kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Ukonga na baadae Mwenge utapelekwa na kukesha katika Chuo cha Kampala kilichopo Gongo la Mboto.

Mpogolo alisema mradi wa nishati safi katika Soko la Ferri unatarajia kuwanufaisha wakaanga samaki wapatao 48 kitakachowezesha kila mmoja kuwekewa mita yake ni mwendelezo wa mkakati wa kutumia nishati safi ili kulinda mazingira ambao uliasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambapo hadi sasa jumla ya mitungi 1,541 imegaiwa kwa Mama na Baba lishe na zaidi ya Taasisi 210 zenye uwezo wa kuhudumia watu zaidi ya 100 zimehamasishwa kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Amefafanua malengo ya mradi huo ni kupunguza matumizi ya nishati inayotokana na miti na mkaa ambayo inachangia katika uharibifu wa mazingira, Kupunguza gharama za uendeshaji kwa wajasiliamali na kuounguzanathari za kiafya zitokanazo na nishati chafu.

Amefafanua Wilaya ya Ilala imewezesha kutekeleza miradi hiyo kwa kuletewa fedha nyingi na Rais ambazo zimetokana na mapato ya ndani.

Kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa 2025 Ismail Ussi alisema Ujumbe Mkuu wa Mwenge wa Uhuru mwaka huu ni “Jitokeze kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu”.

Ussi amesema mbio hizo za Mwenge kitaifa zimebeba ujumbe za kuelimisha jamii ya  watanzania katika kutokomeza maradhi mbalimbali zenye jumbe mbalimbali ikiwemo VVU/UKIMWI, chini ya kauli Mbiu “Chagua Njia Sahihi, Tokomeza UKIMWI uishi salama.

Amesema mbio hizo ni pamoja na kusimamia na kukagua utekelezaji wa  maono ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwenda kuwanufaisha wananchi kiuchumi, kuboresha sekta ya afya, miundombinu ya barabara, maji nanmengine ambayo yanatakiwa yatekelezeke.

"Mimi kama kiongozi wa mbio za Mwenge nawaasa viongozi wasimamie miradi hiyo kwa kuilinda ili kufanikisha maono ya Rais kusaidia wananchi wake" amesema