ZIKIWA zimepita siku sita tangu kuripotiwa tukio la kupotea kwa mfanyabiashara, Daisle Ulomi, mkazi wa Mikocheni jijini Dar es Salaam, amekutwa amefariki na mwili wake kuhifadhiwa katika Hospitali ya Rufani Mwananyamala.
Ulomi alikuwa ni mfanyabiashara wa fedha za mitandao ya simu eneo la Sinza Kijiweni na Mwenge, alipotea katika mazingira yenye utata Desemba 11, mwaka huu alipomuaga mke wake anakwenda kufuatilia mzigo bandarini.
Akizungumza na Nipashe, baba mkwe wa Ulomi, Japhet Munisi, alisema mke wa marehemu alipigiwa simu jana kutoka hospitali na kuambiwa kwamba kuna mwili umeonekana uko katika chumba cha kuhifadhia maiti (mochwari).
Alisema, alikwenda, hospitalini na kuukagua mwili huo na kuutambua kuwa ni wa Ulomi.
“Tulipata taarifa hizi majira ya saa 7:00 mchana kwamba kuna mwili uko mochwari, ilibidi niende mimi Hospitali ya Mwananyamala kwa sababu ndugu wengine wako nje ya Dar es Salaam na nilithibitisha kuwa ni Ulomi, kwa sasa wanafamilia wanakaa kujadili kwamba atazikwa Moshi au wapi,” alisema Munisi.
Aidha, baada ya kuthibitisha kuwa ni Ulomi aliwauliza wahudumu wa hospitali, lakini hawakutaka kumpa maelezo ya kina kwamba mwili huo ulifikaje eneo hilo.
“Niliwauliza askari waliokuwapo eneo hilo kwamba mwili wa Daisle umefikaje hospitali, wakasema wanafanya uchunguzi kwanza ndipo watatoa taarifa,” alisema Munisi.
Taarifa zilizopatikana mitandaoni, zilieleza kuwa siku hiyo (Desemba 11), Ulomi aliondoka Sinza Kijiweni saa sita mchana, aliaga kuwa anakwenda Mbagala, bandari kavu kukagua kontena lake baada ya kuitwa na watu waliodai walikuwa wanashughulikia kulitoa bandarini.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa Ulomi aliondoka ofisini kwake akiwa na usafiri wa pikipiki akiendesha mwenyewe na tangu siku hiyo hakuonekana tena hadi mwili wake ulipopatikana akiwa amefariki.
Nipashe lilimtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro na alipopigiwa simu ilipokewa na msaidizi wake na kueleza kuwa kamanda (Muliro) yuko kwenye kikao, lakini kuhusu suala hilo uchunguzi unaendelea na utakapokamilika taarifa kamili zitatolewa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED