Mzee aliyeishi na VVU miaka 32 anena magumu aliyopitia

By Nebart Msokwa , Nipashe
Published at 11:44 AM Dec 01 2025
Mzee Douglas Kisunga (72), mkazi wa Isanga jijini Mbeya.

LEO dunia inaadhimisha Siku ya UKIMWI Duniani tangu kuanzishwa kwake mwaka 1988, ikiwa ni miaka 37 sasa ya kampeni za kupambana na janga hili linaloendelea kuathiri mamilioni ya watu.

Kaulimbiu mbalimbali zimekuja na kupita, lakini lengo limebaki lile lile: kuzuia maambukizi mapya, kulinda waliokuwa katika hatari na kuwezesha jamii kuishi na watu wenye Virusi vya UKIMWI (VVU) bila unyanyapaa.

Katika kuadhimisha siku hii muhimu, simulizi ya Mzee Douglas Kisunga (72), mkazi wa Isanga jijini Mbeya, inaibuka kama moja ya hadithi za kipekee zinazovunja hofu na kuonesha kwamba kuishi na VVU si hukumu ya maisha kukoma. Ni hadithi ya maisha ya zaidi ya miaka 32 ya ujasiri, uamuzi mgumu na mapambano ya kibinadamu.

 HOFU ILIPOANZA

Tanzania ilipogusia kwa mara ya kwanza kuwapo maambukizi ya VVU mapema miaka ya 1980, hofu ilikuwa juu kuliko uelewa. Rais wa wakati huo, Hayati Ali Hassan Mwinyi, alitangaza kuwa ni janga la kitaifa na kwa kweli, jamii ilikumbwa na mshtuko. 

Watu waliokutwa na virusi hivyo walijikuta wakikumbwa na unyanyapaa, wengine wakikataliwa na familia zao na wengi wakiona kwamba mwisho wa maisha yao umefika. Katika hali hiyo ya sintofahamu ndipo safari ya Mzee Kisunga ilipoanza.

Kabla ya mwaka 1993, Mzee Kisunga alikuwa mwalimu wa shule za msingi katika Wilaya ya Mbeya, akiwa ameijenga taaluma yake kwa miaka mingi. Lakini ghafla, mapema mwaka huo, afya ilianza kudorora bila sababu inayoeleweka.

"Nilikuwa ninaumwa, lakini madaktari hawakuweza kuelewa chanzo. Wakanishauri nipime VVU… ilikuwa ni hofu tupu," anasema.

Ilipofika siku ya kupokea majibu, zile dakika chache za kusubiri mtihani mgumu. Hatimaye, alielezwa kuwa ana maambukizi. Ndani yake kulijaa wingu jeusi.

"Nilinyong’onyea. Nilijiona kama nimeshafariki dunia. Niliogopa hata kivuli changu," anasimulia.

Katika mshtuko huo, alichukua uamuzi mzito - akiandika barua ya kuacha kazi yake ya ualimu.

"Nilikata tamaa kabisa. Nilidhani sitafika hata mwisho wa mwaka. Nikajiondoa kwenye kazi, nikakata shughuli nyingi nilizopenda, hata tendo la ndoa niliacha kabisa kutokana na hofu."

 MIAKA 14 BILA DAWA

Kwa miaka 14, kuanzia 1993 hadi 2007, Mzee Kisunga hakuwa akitumia dawa za kupunguza makali ya (ARV), kwani wakati huo dawa hizo hazikuwa zimeanza kupatikana nchini. Aliishi kwa kutegemea ushauri wa kitabibu.

Alizingatia: kula chakula bora, kuepuka ngono zembe, kupumzika vya kutosha na kutunza mwili na afya ya akili.

Ni utaratibu aliouchukua kwa umakini wa hali ya juu na bila kujua, alikuwa anaandaa mwili wake kwa safari ndefu zaidi.

Mwaka 2007, alipima na kugundua kinga zake (CD4) zimeanza kushuka, ndipo akaanza rasmi kutumia dawa.

"Nimetumia dawa sasa kwa miaka 18. Siri ya kuishi muda mrefu ni ufuasi mzuri - kila siku, kwa wakati, bila kukosa," anasema.

 KUTOKUJIFICHA 

Kwa miaka miwili ya kwanza baada ya kupata majibu, Mzee Kisunga alitembea na siri nzito moyoni. Aliumia kimya kimya.

"Ilikuwa siri yangu. Nilijihisi mnyonge. Lakini mwisho nikafahamu siwezi kuishi maisha ya kujificha," anasema.

Mwaka 1995, aliamua kuieleza familia yake. Kipaumbele kilikuwa kujenga uelewa na upendo. Baadaye akawafahamisha majirani, marafiki na hatimaye jamii kwa ujumla.

Uamuzi huo ulimfungulia milango ya kuwa sauti ya watu wanaoishi na VVU (WAVIU). Tangu wakati huo, amekuwa mchangiaji katika mikutano ya kitaifa na kimataifa, mwezeshaji elimu ya VVU/UKIMWI, mwongozo kwa vijana na watu wanaoanza safari ya dawa na mjumbe wa kampeni mbalimbali za kutokomeza UKIMWI.

"Kwa sasa niko huru. Nimefundisha, nimezunguka nchi, nimehubiri matumaini. Nilipoteza ualimu wa darasani, lakini nimekuwa mwalimu wa jamii nzima," anasema.

 AFYA NA MAZINGIRA

Mzee Kisunga anatoa wito wa kuelewa kwamba UKIMWI si hukumu. Anapinga unyanyapaa, analaani kauli potofu za waganga wa jadi na "manabii wa miujiza" wanaodai kuponya UKIMWI.

"Hakuna dawa ya kumaliza virusi duniani kote. Hakuna maombi yanayobadili hilo. Tusidanganyike. Dawa pekee zinazofanya kazi ni ARV, tena zikinywewa kwa usahihi," aonya.

Anasema mtu anayefuata dawa kikamilifu, virusi vinashuka hadi chini ya kiwango cha kutambulika, hawezi kumwambukiza mtu mwingine na anaweza kuishi maisha marefu kama mtu mwingine yeyote.

Anaonya kuwa kwa mtu ambaye hafanyi ufuasi mzuri, virusi vinaongezeka, kinga hushuka, huwa rahisi kupatwa na magonjwa sugu na anaweza kuzalisha virusi visivyoathirika na dawa.

 SIKU YA UKIMWI 

Katika maadhimisho ya mwaka huu, hadithi ya Mzee Kisunga inasimama kama mwanga wa matumaini na ukumbusho kwamba UKIMWI si hatima. 

Wataalam wanasema Tanzania inaweza kufikia malengo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya kutokomeza UKIMWI kufikia mwaka 2030 ikiwa watu wote watapima afya zao mara kwa mara, walio na maambukizi wataanza dawa mapema, watatumia dawa bila kukosa, jamii itaondoa unyanyapaa na vijana watajikinga na maambukizi mapya.

Mzee Kisunga anasisitiza: "Tusiangalie tu njia za maambukizi. Kila mmoja apime afya yake. Kama una maambukizi, kuanza dawa si mwisho wa dunia. Mimi ni mfano hai, nimeishi zaidi ya miaka 32."

 UJUMBE MAALUMU 

Kwa vijana, Mzee Kisunga anatoa nasaha nzito: "Epukeni ngono zembe, tumia kinga sahihi wakati wote na tambueni kuwa maisha ni safari ndefu inayohitaji umakini."

 Kwa wazazi, Mzee Kisunga anasema: "Wasaidieni watoto kupima na kujua hali zao, tumieni muda kuelimisha badala ya kutisha na ondoeni unyanyapaa majumbani."

Mzee Kisunga anaongeza: "Sikuiona miaka kumi mbele. Lakini leo nipo hapa, nikiwa bado mwalimu wa maisha. Nikikumbuka nilivyoogopa, ninajua kila mtu anaweza kuishi zaidi ya alivyotarajia, akitunza afya, akifuata dawa, akijitunza na akipendwa."