NI neema tu. Vijana 60 kutoka Kata za Kahe Magharibi, Mbokomu (Wilaya ya Moshi), Biriri na Ivaeny (Wilaya ya Siha), mkoani Kilimanjaro, wamewezeshwa kupata fursa rasmi za ajira, wakiwamo wasichana 36, sawa ana asilimia 60 na wavulana 24, sawa na asilimia 40.
Huku wanufaika 184, sawa na asilimia 77.3 ya wanavikundi wa VICOBA (Benki za Maendeleo za Vijiji), vinavyohusisha moja kwa moja wanawake, vikishuhudia namna walivyofanikiwa kuongeza mtaji wao wa kibiashara kwa wastani wa asilimia 20.
Ofisa Ufuatiliaji na Tathimini wa Shirika la Maendeleo ya Jamii la TUSONGE CDO, Gilbert Owen, akizungumza leo katika kikao kazi cha wadau kilichoketi kufanya tathimini na kutoa mapendekezo yao, kabla ya kufungwa kwa mradi wa uchumi, amesema watu hao waliguswa na neema hiyo kati ya mwaka 2023/2025.
Kuhusu suala la kuimarisha ushiriki wa wanawake na haki za umiliki, amesema wanawake 198, sawa na asilimia 83.2 wameripoti kumiliki angalau aina moja ya mali kisheria, huku wanawake 117, sawa na asilimia 49.2 wamekuwa wawakilishi kwenye majukwaa mbalimbali ya uongozi au maamuzi.
Mradi huo wa uchumi, ulikuwa ukilenga zaidi kuboresha hali ya mapato ya wajasiariamali wadogo, kuimarisha ushiriki wa wanawake na haki za umiliki na kuboresha kinga na ushawishi wa ukatili wa kijinsia (GBV).
Kwa mujibu wa Owen, katika kuboresha kinga na ushawishi wa ukatili wa kijinsia, kesi 171 sawa na asilimia 71.8 zilinakiliwa kwa kutumia mbinu ya kumweka mlengwa na Kamati za MTAKUWWA (Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto).
“Tulisema angalau kiashiria kifikie asilimia 30 ya waendesha bodaboda na viongozi wa dini walijihusisha kikamilifu katika kupinga ukatili wa kijinsia kwa kutoa elimu au msaada kwa waathirika wa GBV katika jamii za Kahe Magharibi, Ivaeny, Mbokomu na Biriri. Sasa ushiriki wake umefikia asilimia 171.8,”amesema.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TUSONGE CDO, Aginatha Rutazaa, akizungumza na wadau hao ameeleza:
“Nikiangalia nilipoanza Januari 2025 na sasa hivi namaliza Desemba, bila hiki kitu nisingekuwa hapa nilipo. Haya ndio mambo tunayotaka tuyazungumze. Yako mafanikio mengi mengi na yako yakufichua mnataka yafanyike vipi kama mradi utaendele.”
Kiongozi wa mila wa jamii ya kifugaji ya Kimasai, Mailoji Mollel, Mkazi wa Mawala, alisema anatamani mradi huo kama utaendelea, waongeze nguvu katika elimu ya uchumi na uwekezaji.
“Rasilimali watu yenye ujuzi, ubunifu na maadili ndiyo msingi wa kujenga uchumi jumuishi unaowanufaisha Watanzania wote,”amesema Mollel.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED