“Niko tayari kuitwa kuhojiwa kuhusu umiliki Lake Oil”

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 01:43 PM Nov 28 2025
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Ridhiwani Kikwete.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Ridhiwani Kikwete, amesema yuko tayari kuitwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ili ajibu tuhuma zinazomhusisha na umiliki wa vituo vya mafuta vya Lake Oil.

Akizungumza na watumishi wa wizara yake Novemba 26, 2025, Ridhiwani amesema uwazi kwa viongozi wa umma ni muhimu  na kwamba pale kunapojitokeza tuhuma au sintofahamu  ni wajibu wa mamlaka husika kufanya uchunguzi na kuweka ukweli hadharani.

“Malalamiko juu ya viongozi yamekuwa mengi, haijulikani lipi ni kweli na lipi si kweli, ni muhimu uchunguzi ufanyike na taarifa zikawekwa wazi,” amesema.

Amebainisha kuwa maandamano yaliyotokea  wakati wa uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025 yalibeba malalamiko kuhusu maadili ya viongozi, ikiwamo madai kuwa vituo vya mafuta vya Lake Oil vinamilikiwa naye.

“Kuna mtu anaitwa Ali Edha ana vituo vya mafuta vinavyoitwa Lake Oil, lakini vimechomwa moto kwa madai kuwa ni vya Ridhiwani,” amesema.

Ridhiwani aliitaka Sekretarieti ya Maadili isiogope kumuita, akisisitiza kuwa yuko tayari kuhojiwa wakati wowote. Pia alipendekeza uchunguzi ufanyike kwa kina na baadaye matokeo yake yawasilishwe hadharani kupitia mkutano na waandishi wa habari.
Ameishauri tume hiyo pia kuiomba jamii kutoa ushahidi wa ziada, ili kurahisisha kuthibitisha ukweli wa tuhuma hizo.

Dk.Mwigulu: Sisi si wamiliki wa mabasi ya Esther

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, akihutubia wananchi mkoani Singida, alikanusha madai kuwa yeye na mkewe wanamiliki mabasi ya Kampuni ya Esther, ambayo baadhi yalichomwa moto wakati wa vurugu za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Amesema taarifa hizo ni za uzushi na zimekuwa zikitumiwa kuchochea taharuki na chuki kwa viongozi wa serikali.