Polepole atimiza siku 65, Mdude 222 bila kuonekana

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:20 AM Dec 11 2025
Polepole atimiza siku 65, Mdude 222 bila kuonekana
PICHA: MTANDAO
Polepole atimiza siku 65, Mdude 222 bila kuonekana

Ikiwa tunaeleka ukingoni mwa mwaka 2025, leo zimetimia siku 223 tangu kutekwa kwa kada wa Chama cha Demokrasia na Maendelo (CHADEMA) Mdude Nyagali na watu wasiojulikana usiku wa Mei 2 mwaka huu akiwa nyumbani kwake mkoani Mbeya.

Kwa mujibu wa mkewe, Sije Mbugi aliyesimulia tukio hilo na kunukuliwa na vyombo vya habari, anasema wakiwa nyumbani kwao Mtaa wa Iwambi, Jijini Mbeya walisikia sauti za watu wakijaribu kufungua geti, yeye akiwa wa kwanza kusikia alimuamsha na mumewe baada ya muda mfupi walifanikiwa kuvunja geti kisha mlango wa chumba walicholala na kuingia ndani. Yeye na mumewe anaeleza walijitahidi kupambana lakini walizidiwa nguvu na watu hao ambao walifanikiwa kumchukua Mdude na kuondoka nae kusikojulikana na hadi leo haijulikani alipo.

Hali ikiwa hivyo kwa Mdude Nyagali, aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole yeye inadaiwa alivamiwa na watu wasiojulikana usiku wa Oktoba 6 mwaka huu huku picha zikisambaa mitandaoni zikionesha nyumba yake ikiwa imevunjwa milango huku michirizi ya damu ikionekana sakafuni kuonesha huenda palikuwapo ya kujitetea dhidi ya watekaji na hivyo kujeruhiwa. Tangu wakati huo zimetimia siku 65 bila Polepole kuonekana hadharani huku Jeshi la Polisi nchini likiahidi kuendelea kufuatilia matukio hayo kwa karibu ili kuyadhibiti.