Prof. Lipumba awaangukia watanzania wamchangie kwenye uchaguzi mkuu

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 03:31 PM Apr 07 2025
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa Prof. Ibrahim Lipumba
Picha: Mtandao
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa Prof. Ibrahim Lipumba

MWENYEKITI wa chama cha Wananchi, Prof. Ibrahim Lipumba, amesema kwa kuwa shughuli za uchaguzi kuna gharama, anatoa wito kwa wanachama na wananchi kwa ujumla, kukichangia chama hicho.

Amesema katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu pia ni wito kwa wananchi kuendelea kujiunga na CUF na kujitokeza kugombea nafasi za udiwani, uwakilishi, ubunge, pamoja na urais Zanzibar na Tanzania bara.

Prof. Lipumba amesema hayo jana, Dar es Salaam, Aprili 6, mwaka huu, katika taarifa yake kwa umma kupitia vyombo vya habari juu ya mtazamo wa CUF kisiasa na kiuchumi.

“Kushiriki katika uchaguzi kuna gharama. Tunatoa wito kwa wanachama na wananchi kwa ujumla kukichangia Chama kwa hali na mali kiweze kushiriki kikamilifu kwenye Uchaguzi Mkuu.

“Mwaka huu ni wa Uchaguzi Mkuu. Ni muhimu Uchaguzi huuukawa huru na wa haki na tusirudie yaliyofanyika katika Uchaguzi Mkuu Mwaka 2020 au Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 na 2024. 

“Ni muhimu kwa haraka iwezekanavyo Rais (Samia Suluhu Hassan), akutane na wadau muhimu wa uchaguzi kufikia mwafaka wa kuhakikisha Uchaguzi wa 2025 unakuwa huru na wa haki.

Mtaalamu huyo wa uchumi, amesema msimamo wa CUF ni kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa, baada ya uchaguzi kukamilisha upatikanaji wa Katiba inayotokana na maoni ya wananchi, kuweka mikakati ya kutekeleza mipango na programu za taifa zitakazofanikisha ndoto ya Watanzania.

“Lengo ni kuwa na nchi yenye haki sawa kwa wote na iliyofanikiwa kutokomeza umasikini na kumhakikishia kila mwananchi ana kipato cha msingi cha kukidhi mahitaji yake muhimu.”