PSSSF kuendelea kuwekeza kwenye maeneo salama yenye tija

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 12:08 AM Jul 08 2025
Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji  na Miradi PSSSF, Fortunatus Magambo
Picha: Elizabeth Zaya
Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi PSSSF, Fortunatus Magambo

MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), umewekeza maeneo salama yenye kuuwezesha kupata faida kubwa ikiwamo hatifungani na dhamana za serikali na kwamba kwa mwaka wa fedha uliomalizika umepata faida ya Sh. trilioni 1.3.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji  na Miradi PSSSF, Fortunatus Magambo kwenye banda la Mfuko huo kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam(DITF), yanayoendelea kwenye viwanja vya Julius Nyerere, maarufu Sabasaba.

Amesema asilimia 84 ya uwekezaji uliofanywa na mfuko huo umewekwa maeneo hayo ya hati fungani ambako kuna uhakika yanayouwezesha mfuko kupata faida kubwa na kulipa wastaafu na wanachama wake mafao mazuri na endelevu.

“Tumewekeza maeneo salama ambayo yanaleta faida kubwa kwa wakati ili tuweze kulipa mafao bora kwa wastaafu wetu na wanachama, ndiyo maana asilimia 84 ya uwekezaji wetu tumeuwekeza kwenye amana za serikali na hati fungani,” amesema Magambo.

“Tunapokea wafanyakazi wapya kila siku na wengine wanastaafu kwa hiyo wakistaafu wanapaswa wakutane na pensheni yao, na ili iwe hivyo lazima tuwekeze fedha zao kwenye maeneo sahihi yenye faida ya haraka na ya uhakika, na uwekezaji huu unafuata miongozo ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Amewahakikishia wanachama wa PSSSF wakiwamo wastaafu kuwa Mfuko uko salama na una ukwasi wa kutosha kuhakikisha mafao yanalipwa kwa wakati siku zote.

Amesema PSSSF imekuwa ikijenga nyumba za bei nafuu Tanzania nzima na lengo la kuwa na bei nafuu ni kuhakikisha wanachama wa mfuko huo wanapostaafu kama hawajajenga nyumba wapate nyumba na ambao hawana viwanja wapate viwanja.

“PSSSF tuna ofisi kila mkoa kwa hiyo nawahamasisha wanachama wetu  na wastaafu watarajiwa wafike kwenye ofisi zetu waulize nyumba na viwanja waweze kukopa, sisi tunataka mstaafu wetu waishi maisha mazuri baada ya utumishi wao ndiyo sababu ya kujenga hizi nyumba za gharama nafuu,” amesema.

Amesema mfuko umewekeza kwenye majengo mengi ya kisasa likiwamo jengo lililopo barabara ya Sam Nujoma lenye  gorofa 33 ambalo ni bora kwa Afrika Mashariki na Kati kutokana na kujengwa kisasa.

Kagaruki amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara ambayo yamesababisha jengo hilo refu zaidi kupata wateja kwa asilimia 80.

“Kupata asilimia 80 ya wateja kwenye jengo kubwa kama lile siyo jambo jepesi inamaana kuna kazi kubwa imefanyika na hapa lazima Rais Samia Suluhu Hassan apewe maua yake kwa kuweka mazingira mazuri yaliyovutia wawekezaji kumiminika nchini,” amesema.

Amesema PSSSF imekuwa ikijitahidi kujenga majengo yenye ofisi zenye ubora wa kimataifa ili kuwawezesha wawekezaji wanaokuja kuwekeza nchini kupata ofisi zenye hadhi ya kimataifa.

“Maana yetu ni kuhakikisha mwekezaji anapokuja hapa apate ofisi ambayo inafanana na ofisi yake ya China au iliyoko Marekani na kwingineko, tunataka apate huduma zile zile ndiyo maana wawekezaji wanazidi kuja nchini kwa kuona ni sehemu salama na sahihi ya kuwekeza,” amesema.

Kuhusu eneo la viwanda, amesema PSSSF imeunga mkono jitihada za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kwa kuwekeza kwenye viwanda vikubwa viwili ambavyo vimeonyesha mafanikio makubwa

Ametaja viwanda hivyo kuwa ni kiwanda cha viatu Karanga International Lather Industry kilichoko mkoani Kilimanjaro ambacho kinatoa viatu bora vinavyouzwa ndani na nje ya nchi.

Kiwanda kingine amesema ni cha nyama ambacho kimeongeza ajira kwa watanzania wengi na kuongeza kipato cha wafugaji ambao wamekuwa wakipeleka mifugo yao kuuza kwenye kiwanda hicho.