PURA yaendelea kutoa elimu Sabasaba fursa sekta ya mafuta, gesi

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 12:16 AM Jul 08 2025
Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wazawa na Uhusishwaji wa Wadau kutoka PURA, Charles Nyangi
Picha: Elizabeth Zaya
Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wazawa na Uhusishwaji wa Wadau kutoka PURA, Charles Nyangi

MAMLAKA ya Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA, imesema itaendelea kuwaunganisha watanzania katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi zinazohusisha ushiriki wa wazawa (local content) katika kuongeza mnyororo wa thamani wa bidhaa na huduma za ndani ya nchi.

Akizungumza na Nipashe katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF), Mkurugenzi Mkuu wa Pura, Charles Sangweni amesema jukumu hilo linatokana na umuhimu wa kuwaandaa Watanzania kufanya kwa kina shughuli za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi zaidi ya ilivyo sasa.

Amesema watahakikisha wanawajengea uwezo na kuwapa taarifa sahihi kuhusu kuongeza mnyororo wa thamani wa bidhaa na huduma zao na kuchangamkia fursa katika miradi inayotekelezwa na kampuni kubwa kwa usimamizi wa PURA.

Sangweni amesema watanzania wana fursa katika usafirishaji, vyakula na ushiriki wa kazi hizo kwa kuajiriwa na kuwa mbia akisisitiza kwamba ubia ni takwa la lazima ambapo wazawa anashirikiana na kampuni za kigeni kwa asilimia 25.

Amesema tangu PURA ianze shughuli zake mwaka 2015, tayari ina kampuni tisa inazozisimamia katika uendeshaji wa shughuli hizo za mafuta na gesi asilia ikiwamo ya TPDC ambayo ni ya Tanzania na nyingine zote ni za nje. 

Mkuu wa Kitengo cha Ushiriki wa Wazawa na uhusishwaji wa wadau wa PURA, Charles Nyangi, amesema Mamlaka hiyo tayari ina kanzidata maalum  inayowaunganisha watoa huduma wazawa na wageni ambapo kila kampuni ya kigeni ya kutafuta na kuchimba mafuta na gesi itapaswa kuwapata watoa huduma kutoka humo.

Ametoa wito kwa watanzania kutumia fursa ya uwapo wa maonesho hayo kwenda kujifunza shughuli zinazohusisha sekta hiyo ya mafuta na gesi.

"Tunaendelea kuwakaribisha wananchi katika banda letu la PURA ili waje wapate fursa ya kujifunza shughuli mbalimbali kuhusiana na utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi lakini pia watapata kujua fursa zinazopatikana katika mnyororo wa mafuta gesi.

"Wapate kujua my fursa gani zinazokuwapo, zinaweza kuwa ajira, biashara au uwekezaji ili wachangamkie lakini hii ni rasilimali ya Watanzania wote, wanatakiwa kuifahamu namna inavyopatikana na matumizi yake ni yako na jinsi gani wanaweza kunufaika nayo,"amesema Nyagi.

PURA imekuwa ikishiriki maonesho lengo kubwa ikiwa ni kutoa elimu kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na mamlaka hiyo na namna wanavyoweza kuchangamkia fursa mbalimbali zitokanazo na sekta hiyo ya mafuta na gesi. 

Maonesho hayo ya Kimataifa ya 49 yalianza Juni 28, yanatarajiwa kufungwa rasmi Julai 13 mwaka huu.