PSSSF yatoa mil 10 mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kupitia NBC Marathon

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:32 PM Jul 15 2024
Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF),Yesaya Mwakifulefule (kulia) akimkabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni 10, Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano benki ya NBC, Godwin Semunyu.
Picha: Mpigapicha Wetu
Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF),Yesaya Mwakifulefule (kulia) akimkabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni 10, Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano benki ya NBC, Godwin Semunyu.

MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), umetoa msaada wa shilingi milioni 10 kuchangia mapambano dhidi ya ya Saratani ya Shingo ya Kizazi kwa akina mama kupitia mbio za NBC Marathon.

Akikabidhi msaada huo Julai 15, 2024 kwenye Makao Makuu ndogo ya PSSSF jijini Dar es Salaam, Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, Yesaya Mwakifulefule, amesema PSSSF kama taasisi ya umma, imetoa mchango huo ili kusaidia kampeni ya serikali ya mtu ni afya.

“Sisi kama PSSSF tunao wanachama wetu wengi nchi nzima, tungefanya sisi peke yetu tungehitaji fedha nyingi kufanikisha jambo hilo, lakini wenzetu wako mstari wa mbele kufanikisha ajenda ya serikali ya mtu ni afya, wafanyakazi 180 wa PSSSF watashiriki kwenye mbio hizo za NBC Marathon jijini Dodoma.” amefafanua.

Akitoa neno la shukrani, Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano NBC, Godwin Semunyu, ameishukuru PSSSF kwa msaada huo ambao sio tu utakwenda kuwasaidia akina mama, bali pia utakwenda kutoa ufadhili kwa wakunga.

“Lengo la mbio za NBC Marathon ni kukusanya fedha ili kusaidia mapambano dhidi ya Saratani ya Shingo ya Kizazi kwa akina mama na Kutoa ufadhili wa masomo kwa Wakunga ili kupunguza upungufu wa wakunga nchini.” amesema Semunyu.

Mbio za NBC Marathon zinatarajiwa kufanyika Julai 28, 2024 jijini Dodoma.