Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk. Ashatu Kijaji, amesema kuwa hatua ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kuidhinisha kiasi cha Shilingi bilioni 216 kwa ajili ya ruzuku ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo, ni ushahidi tosha wa upendo mkubwa alionao kwa wafugaji nchini.
Dk. Kijaji aliyasema hayo Julai 3, 2025, wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha, wakati wa hitimisho la ziara yake ya kukagua utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya chanjo na utambuzi wa mifugo, ambapo jumla ya mifugo 4,281 ilichanjwa na kutambuliwa.
“Tayari Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ameshatoa Shilingi bilioni 65 kwa ajili ya kufanikisha zoezi hili kwa mwaka huu. Hii ni fursa kwa wafugaji wetu kwani tayari kuna soko la kimataifa linalohitaji tani 50,000 za nyama kutoka kwa mifugo iliyochanjwa na kutambuliwa,” alisema Dk. Kijaji.
Waziri huyo alibainisha kuwa kampeni hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Miaka Mitano wa Uboreshaji wa Sekta ya Mifugo, ulioasisiwa na Rais Samia. Mpango huo unalenga kuwainua wafugaji kiuchumi kwa kupitia ufugaji wa kisasa unaokidhi mahitaji ya masoko ya kimataifa.
Dk. Kijaji aliongeza kuwa kampeni hiyo ya kitaifa ilizinduliwa rasmi na Rais Samia Juni 16, 2025, wilayani Bariadi mkoani Simiyu, na itaendelea kutekelezwa katika mikoa mingine ikiwemo Mara, Simiyu, Geita, Pwani, Morogoro, Tabora na Dodoma.
“Kupitia kampeni hii, tunakwenda kubadilisha maisha ya wafugaji nchini kwa kuhakikisha mifugo yao inakuwa na thamani zaidi, afya bora na uwezo wa kuuzwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi,” alisisitiza Waziri Kijaji.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED