Simba kumpa mkataba kocha Fadlu, waganga yajayo

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 02:22 PM Jul 04 2025
news
Picha Mtandao
Kocha wa Simba Davids Fadlu

Baada ya kikao cha juzi jioni cha Washauri, Bodi ya Wakurugenzi chini ya Mwenyekiti wake, Mohamed Dewji, klabu ya Simba imefanya maamuzi kadhaa kwa ajili ya kujipanga kuelekea msimu ujao.

Bodi hiyo ilikutana kufanya tathimini ya msimu uliopita pamoja na kuweka mikakati kuelekea kwenye msimu ujao wa mashindano ya ndani na yale ya kimataifa.

Moja ya maamuzi waliyoyachukua ni kumuongezea mkataba kocha wao, Davids Fadlu na baadhi ya wachezaji hukupia ikipitisha panga kwa wachezaji ambao hawapo kwenye mipango ya kocha huyo.

Mkataba wa awali wa Fadlu ulikuwa umemalizika mwezi uliopita baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja akitokea Raja Casablanca ya Morocco.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho, zinasema Fadlu atapewa mkataba mpya baada ya bodi hiyo kuridhishwa na uwezo wake na kufanikiwa kwenye mbinu na nidhamu ya timu.

“Uongozi wa Simba umeonyesha kuridhishwa na utendaji wake hasa kwa jinsi alivyoimarisha kikosi, nidhamu na mbinu, ingawa Simba hatukuchukua taji lolote, maende leo ya kiuchezaji yalionekana katika kipindi chake.

Alisaini mkataba wa mwaka mmoja tu, lakini pia kikao kimepitisha maamuzi ya usajili, wasajiliwe wachezaji wenye uwezo mkubwa lakini pia wale ambao hawapo kwenye mipango kutokana na kushuka kiwango wataachwa,” alisema mtoa taarifa ndani ya klabu hiyo.

Alipoulizwa Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, juu ya taarifa hizo, alisema kocha mwenyewe Fadlu pia alionekana kupendelea kubaki na Simba licha ya klabu nyingi za nje kumuhitaji.

“Kocha mwenyewe anaitaka Simba, amekwenda mapumzikoni na atarejea mwishoni mwa mwezi huu tayari kwa kuanza msimu mpya. Mambo yote yapo sawa,” alisema Ahmed.

Alisema moja ya mambo yaliyojadiliwa ni tathimini ya msimu uliopita, lakini kuandaa mpango mkakati wa kufanya usajili bora kwa ajili ya msimu ujao.

“Bodi ya Wakurugenzi chini ya Mo, na Makamu Mwenyekiti, Murtaza Mangungu, ilikutana pamoja na Bodi ya Washauri kufanya tathmini kuangalia tumefaulu wapi tumefeli wapi.

Baada ya hapo tumeweka mikakati ya siri, umewekwa mpango kuelekea kwenye kipindi cha usajili, kilichojadiliwa kikubwa katika usajili ni kwamba tunavamia namna gani soko la usajili, tunaboresha vipi kikosi chetu ili tupambane zaidi.

Tumefanikiwa eneo la kujenga timu, lakini tumefeli kwa kukosa makombe yote, kwa hiyo mipango iliyopo ni kuhakikisha msimu ujao tunaongeza ubora wa kikosi ili kutwaa mataji,” alisema Ahmed.

Aidha, alisema suala la wachezaji gani wataachwa, mashabiki na wanachama wa klabu hiyo watajua siku za mbele. Simba imekosa mataji yote iliyokuwa ikipigania msimu huu, ikianzia na Ngao ya Jamii, Kombe la Shirikisho Afrika, Ligi Kuu, pamoja na Kombe la FA.