Fountain Gate, Stand United uso kwa uso ‘play off’ leo

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 02:36 PM Jul 04 2025
news
Picha Mtandao
Wachezaji wa vikosi vya Fountain Gate na Stand United.

Baada ya kuchapwa jumla ya mabao 4-2 na Tanzania Prisons katika mchezo wa kwanza wa ‘play off’, timu ya Fountain Gate, leo itashuka kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga, kujaribu bahati yake ya kutaka kusalia kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kucheza mechi nyingine ya mchujo dhidi ya Stand United.

Katika ‘play off’ ya kwanza, ililazimishwa sare ya bao 1 -1 nyumbani, Tanzanite Kwaraa, Manyara kabla ya kuchapwa mabao 3-1 ugenini na kuwafanya maafande wa Tanzania Prisons kusalia Ligi Kuu, wenyewe wakilazimika kucheza mechi nyingine ya mchujo dhidi ya timu ya ‘Champioship’ (Stand United).

Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Issa Mbuzi, alisema hawajakata tamaa ya kusalia Ligi Kuu kwani wana dakika zingine 180 ambapo leo watakuwa na dakika 90, kabla ya Jumatatu kumalizia 90 nyingine kwenye mchezo wa marudiano kwenye uwanja wa Tanzanite Kwaraa za kuhakikisha timu yao inasalia Ligi Kuu.

“Tunapaswa tuinue vichwa vyetu juu kwa sababu mapambano bado yanaendelea, tuna dakika 180 za kuibakisha timu Ligi kuu, naamini tutafanya vyema kwenye mchezo huu, baada ya mchezo wa marudiano tutarejea nyumbani kwenye mchezo wa marudiano,” alisema Mbuzi.

Kocha wa Stand United, Juma Masudi, amesema maandalizi ya mchezo yamekamilika na kinachosubiriwa ni mchezo wenyewe ili kujua nani ataibuka na ushindi.

“Tumeshafanya kila kitu kilichotakiwa kufanyika kukabiliana na Fountain Gate, ni matumaini yangu tutafanya vizuri siyo kwenye mchezo wa leo tu hata wa marudiano, tunakwenda kwenye mchezo wa leo kwa kumheshimu mwenzetu kwa sababu yeye yupo Ligi Kuu na sisi tumetoka Champioship.

Stand United ikipata ushindi wa jumla, itapanda Ligi Kuu, ikiiacha Fountain Gate ikishuka daraja, ikipoteza itabaki Championship, ikiwafanya pia wapinzani wao kubaki Ligi Kuu.