Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi, juzi usiku alitangazwa rasmi kuwa atakiongoza kikosi cha Ismailia ya Misri kwenye msimu ujao ya mashindano, siku chache tu baada ya kuwapa Wanajangwani hao mataji mawili ya Ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la FA.
Awali ilielezwa mabosi wa Yanga kugawanyika katika maamuzi ya ama wamuongeze mkataba kocha huyo au waachane naye, lakini jana klabu ya Ismailia ilimtangaza kuwa kocha wake mkuu.
Inaelezwa sababu ya kocha huyo kuamua kuondoka Yanga ni kumalizika kwa mkataba wake wa miezi sita lakini pia ofa nono aliyopewa na waarabu hao wa Misri huku viongozi wa Yanga wakisuasua kufikia mwafaka.
Habari kutoka vyanzo mbalimbali nje ya nchi, vinasema kuwa klabu za USM Alger, CS Constantine, JS Kabylie zote za Algeria na RS Berkane ya Morocco, zilikuwa zinamuwania kwa kuweka dau nono mezani.
Kocha huyo katika klabu yake mpya ya Ismailia, inaelezwa atapokea mshahara mara mbili ya ule aliokuwa akiupokea akiwa Yanga.
Awali, Miloud, mwenye uraia wa Algeria na Ufaransa, alichukuliwa kama kocha wa kumalizia msimu Yanga baada ya kuondoka kwa Saed Ramovic, ambaye alitimkia nchini Algeria kuifundisha klabu ya CR Belouizdad.
Yanga ilimpa mkataba wa miezi sita tu, akitokea Singida Black Stars ambako alikuwa bado hajaiongoza kwenye mchezo wowote.
Viongozi wa Yanga walimpa mkataba huo mfupi ili Ligi imalizike huku wakiwa kwenye harakati za kusaka kocha mwingine.
Hata hivyo, Miloud alionyesha uwezo mkubwa kwa kuiwezesha Yanga kuendeleza makali yake na kutetea makombe yote ya ndani waliyoshindania.
Inaelezwa baada ya uwezo aliouonyesha, mabosi wa Yanga walianza kufikiria kumpa mkataba mwingine kwa ajili ya kuongoza timu hiyo msimu ujao.
“Mechi za mwisho Yanga ilikuwa ikicheza soka kubwa chini ya Miloud na kufanya mabosi wabishane wampe mkataba mrefu zaidi au waendelee na mchakato wa kutafuta kocha mpya mchakato ambao ulishaanza.
Waliotaka abaki walionekana kuwa na hoja kuwa amekaa muda mfupi, lakini ameivusha Yanga sehemu ngumu na kuipa mataji, unajua kadri muda unavyosogea tumekuwa tunaona utofauti, timu inacheza kwa mbinu hasa pale kati na tunavyojenga mashambulizi na hata tunavyoshambulia.
“Lakini nadhani tulichelewa kufanya maamuzi, amemaliza ligi huku akiwa na ofa nyingine na mwisho wa siku kaamua kuondoka,” alisema mmoja wa viongozi wa Yanga.
Alisema wataanza mapema mchakato wa kumpata kocha mpya atakayeifundisha timu hiyo msimu ujao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED