Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi(PPPC), kimezitaka mamlaka za serikali, wakuu wa idara za serikali na wakuu wa taasisi za serikali za mitaa, kufanya utaratibu wa kuibua miradi ambayo zina uwezo wa kuitekeleza kupitia wadau binafsi.
Amesema kuibua miradi na kuitekeleza kwa kuwashirikisha wadau binafsi ni bora zaidi badala ya kuendelea kuiweka kwenye bajeti za serikali ambazo wakati mwingine zinakuja hazitoshi kutekeleza miradi mikubwa.
Akizungumza na Nipashe ndani ya banda la PPPC kwenye maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaama(DITF) yanayoendelea katika viwanja vya sabasaba, Temeke, Mratibu wa Miradi ya Ubia katika Mamlaka za serikali za Mitaa wa Kituo hicho, , Msoleni Dakawa, amesema kuibua miradi kutarahisisha halmashauri nyingi kuwa na kipato kikubwa cha kujiendesha.
Amesema ili kufanikisha hilo, wanachotakiwa kufanya ni kutenga fedha kidogo kwa ajili ya maandalizi ya nyaraka mbalimbali ya kufanikisha kutekeleza miradi hiyo wanayoibua ili iwe rahisi kuitangaza kwa wadau binafsi au wawekezaji.
"Lakini pia kwa zile taasisi zinazomiliki ardhi ambazo hazina hatimiliki za ardhi zao wajitahidi kuzitengeneza ili iwe rahisi kuitangaza kwa ajili ya uwekezaji,"amesema Dakawa.
Amesema ni halmashauri chache zenye uwezo wa kujiendesha kupitia mapato yake ya ndani lakini kupitia mbinu hiyo ya kuibua miradi na kuitangaza kwa wawekezaji itazisaidia kujiendesha na kuziinua zaidi kimapato.
"Kwa hiyo halmashauri zinatakiwa ziibue miradi ambayo itawavutia wawekezaji na mwisho wa siku itaziongezea mapato ya kujiendesha badala ya kuendelea kutegemea bajeti ya serikali kuu."
Ametaja miradi ambayo inaweza kuibuliwa kwenye halmashauri na kuzitangaza kwa wawekezaji kuwa ni pamoja miradi midogo ya kujenga vituo vya afya, shule binafsi na vyuo, masoko, vituo vya basi, vituo vya magari makubwa, miradi ya kujenga maeneo ya starehe, viwanja vya mpira(sports Arena) na mingine kama hiyo.
Kwa mujibu wa Dakawa, sheria imeweka vigezo kwamba uwekezaji kwenye miradi midogo inayoibuliwa kwenye mamlaka za serikali za mitaa ni Sh.bilioni 50 na mikubwa unaanzia zaidi ya Sh..bilioni 50.
Dakawa ametoa wito kwa wananchi, kutumia fursa ya maonesho hayo yanayoendelea, kwenda kujifunza mambo mbalimbali kwenye na kuangalia namna wanavyoweza kuchangamkia fursa zilizopo kupitia kituo hicho cha ubia.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED