RC Macha acharuka Manispaa ya Kahama kukithiri kwa uchafu

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 07:29 PM Jul 15 2024
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza kwenye kikao cha bodi ya barabara.
Picha: Marco Maduhu
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza kwenye kikao cha bodi ya barabara.

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, ameonyesha kukerwa na Manispaa ya Kahama kukithiri wa uchafu, hali ambayo hatari kutokea magonjwa ya mlipuko kikiwamo kipindupindu.

Amebainisha hayo leo Julai 15,2024 wakati akifungua kikao cha bodi ya barabara.

Amesema miundombinu ya barabara inapaswa kutunzwa pamoja na kufanyiwa usafi,lakini amesikitishwa na Manispaa ya Kahama kukithiri wa uchafu,huku chupa zilizotumika zikitupwa hovyo kwenye mitaro ya barabara.

“Mji wa Kahama ni mchafu sana,machupa yaliyotumika yanatupwa hovyo kwenye mitaro ya barabara,Mkurugenzi chukua hatua kwa watu ambao wanachafua barabara,”amesema Macha.

“Njooni mjifunze kwa wenzenu wa Manispaa ya Shinyanga muone hua wanafanyaje wapo vizuri kwenye masuala ya usafi, na hata walishika nafasi ya kwanza kwa Manispaa zote nchini,”amesema Macha.

Amesema pia Kahama kuna tatizo la uholela wa vituo vya mafuta barabarani, na kwamba hawezi kuingilia suala hilo na kutoa angalizo itolewe mikataba kwa watu ambao wanafanya biashara hizo za vituo vya mafuta ili kutoleta madhara baadae.

Aidha,ametaka pia utunzwaji wa miundombinu ya barabara zikiwamo taa za barabara,kuacha kupitisha mifugo,kufanya biashara kando ya barabara,na kudhibiti magari yenye uzito mkubwa ili kutunza miundombinu hiyo.

1

Katika hatua nyingine amewapongeza Wakuu wa wilaya kwa kuchukua hatua dhidi ya Wakandarasi ambao ni wazembe wanaotekeleza miradi kinyume na makubalinao ya mikataba, na kuwataka waendelee kukaza uzi ili kusimamia kikamilifu fedha za miradi ambazo zinatolewa na Mheshimiwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.

“Nawapongeza TANROADS na TARURA kwa utekelezaji wa miundombinu ya barabara na madaraja,lakini kuna udhaifu kidogo katika kuwasimamia wakandarasi,wanatekeleza kazi zao kinyume na mikataba tena wengine wakorofi kweli,”

“Jitafakalini namna ya kutoa zabuni kwa wakandarasi muacha kuwapatia zabuni hizo bila ya kujiridhisha uwezo wa Mkandarasi,msiwapatia pia kazi wakandarasi wenye kazi nyingi na kusababisha miradi kushindwa kukamilishwa kwa wakati,”amesema Macha.

Ameagiza pia maeneo ambayo miradi ya maendeleo inatekelezwa, mabango hayo yaandikwe kwa lugha ya kiwashili.

Mbunge wa Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo, naye amesisitiza suala la kupewa kazi wakandarasi wasio na uwezo na wenye kazi nyingi kwamba lizingatiwe sababu miradi mingi inakwama kutekelezwa na kukamilishwa kwa wakati.
2

“Mfano Kishapu kuna Miradi ya barabara ya mwaka 2023/2024 bado haijatekelezwa kabisa, na sasa tunakwenda kwenye mwaka mwingine wa fedha 2024/2025 na baadhi ya wakandarasi hawapo Site sababu hawana uwezo na sijui walipewaje kazi ,”amesema Butondo.

Meneja Wakala wa barabara mjini na vijijini (TARURA)Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Avith Theodory, amekiri kwamba uwezo mdogo wa wakandarasi kutekeleza miradi ya barabara ni tatizo na kubainisha kwamba watawasiliana kwenye bodi ambayo hua inawasajili sababu wakija kuomba zabuni na kuonyesha “CV”huonekana wako vizuri lakini kumbe hana uwezo.

Aidha, akwiasilisha taarifa ya mpango wa bajeti ya matengenezo ya barabara kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kwamba walitengewa kiasi cha fedha Sh.bilioni 18.2 lakini wakapokea Sh.bilioni 5.7, huku katika mwaka wa fedha 2024/2025 wakitengewa Sh.bilioni 16.6.

Meneja Wakala wa Barabara Tanzania mkoa wa Shinyanga (TANROADS) Mhandishi Samweli Mwambungu, akiwasilisha taarifa ya matengenezo ya barabara kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kwamba walitengewa kiasi cha fedha Sh.10.6, lakini wakapokea Sh.bilioni 5.5 hadi kufikia juni 30.
3

Amesema kwa upande wa miradi ya kimkakati ambapo uwanja wa Ndege Ibadakuli hadi sasa ujenzi wa eneo la kurukia ndege umefikia asilimia 70 na jengo la abiria asilimia 30, na kwamba barabara ya Kolandoto hadi Mhunze tayari wameshatengewa fedha kuanza ujenzi kilomita 20, huku barabara ya Oldshinyanga- Solwa upembuzi yakinifu ukiwa tayari umekamilika.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa, amesisitizwa suala la uzalendeo kwenye usimamizi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo,pamoja na kuwapatia zabuni wakandarasi wenye sifa.

Aidha katika kikao hicho iliwasikishwa pia ujenzi wa miradi ya TACTIC katika Manispaa ya Shinyanga na Kahama.