Ripoti ya utafiti 2023 yabaini changamoto ufanisi kwa wenye ulemavu

By Christina Haule , Nipashe
Published at 05:36 PM Dec 02 2025
Mkuu wa dawati la watetezi wenye ulemavu kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Emmanuel Majeshi

Mkuu wa dawati la watetezi wenye ulemavu kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Emmanuel Majeshi amesema ripoti ya utafiti wa mahitaji wa mwaka 2023 wamebaini vyama na taasisi za wenye ulemavu kukabiliwa na changamoto zinazodhoofisha ufanisi ikiwemo ukosefu wa uwazi wa majukumu na mgawanyo wa kazi.

Majeshi amesema hayo leo wakati akiongea na vyombo vya habari kuelekea kilele cha kongamano la siku ya wenye ulemavu dunia kinachofanyika kitaifa Desemba 3 mjini hapa ambapo kauli mbiu ya kongamano hilo ni “kuendeleza jamii jumuishi kwa watu wenye ulemavu kwa mustakabali wa ustawi wa jamii”.

Anazitaja changamoto zingine kuwa ni kukosekana kwa ushiriki wa baadhi ya taasisi kwenye masuala ya kisiasa na uhaba wa mafunzo rasmi ya uongozi.

Aidha anasema kupitia dawati la watetezi wa haki za wenye ulemavu (DDI) ndani ya THRDC wanalenga kujenga mfumo madhubuti wa utetezi katika mazingira salama yenye shirikishwaji na yenye kuwajenga kusalama, kitaasisi, kifedha, kijamii na kiteknolojia.

Majeshi anasema wanadumisha jitihada za kufanya uchechemuzi wa sera zinazohimiza ujumuishwaji na ulinzi kwao ili kuhakikisha watetezi wa haki za watu wenye ulemavu (HRDDs) wanapata rasilimali, maarifa na mazingira wezeshi ya kutekeleza majukumu yao.

Mmoja wa washiriki wa kongamano hilo Shariff Makame (mwenye ulemavu wa miguu) anasema wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto nyingi hasa kwa kinamama wenye ulemavu katika nyakati za kujifungua kutokana na kuwa na kipato cha chini kinachokinzana na gharama kubwa za matibabu hospitalini.

Hivyo ameziomba mamlaka husika kuwakumbuka katika nafasi mbalimbali hasa kurahisisha upatikanaji wa ajira kwa watu wenye ulemavu huku wakijitahidi kutenga asilimia kubwa pale wanapotoa ajira iwe ni ya wenye ulemavu.