Samia: Turidhiane kwanza, kisha Katiba Mpya

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:17 PM Dec 02 2025
Rais Dk Samia Suluhu Hassan.

Rais Dk Samia Suluhu Hassan amesema licha yaliyotokea, atasimama kuilinda Tanzania kwa nguvu zote.

Amesema yaliyopita si ‘ndwele, tugange yajayo’(Oktoba 29), kama madai ni Katiba hakuna aliyekataa, kuirekebisha Katiba ya Tanzania.

“Mnakumbuka niliunda Tume ya Haki ya Jinai, ikaenda soma na kuniletea mapendekezo, katika kuyatekeleza yapo mapendekezo ya muda mfupi na kati ambayo asilimia 90 yametekelezwa.

“Lililobaki la muda mrefu ni marekebisho ya Katiba ambayo nilisema tutatekeleza, mkisoma ilani ya CCM nilisema ndani ya siku 100 nitaunda Tume ambayo itafanya maridhiano kisha tutaingia katika Katiba,”

Dk. Samia amesema huwezi kuingia kwenye marekebisho ya sheria za nchi, wakati mpo vipande vipande, lazima watu warudi na kuwa kitu kimoja ili kujua njia sahihi ya Kwenda mbele.

“Hamuwezi Kwenda moja kwa moja kutunga Katiba Mpya wakati kila mtu kavimba mashavu, mtatunga Katiba ipi itaundwa hapa?
“Nimesema kwanza turidhiane kwa sababu mmechafua nchi, nilichofanya mwanzo ni kuunda Tume ya kuangalia kwa undani yaliyotokea, nimewapa miezi mitatu,” amesema Dk Samia.