Serikali kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri na kuajiri wengine

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:36 PM Jun 19 2025
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Daniel Mushi.
Picha:Mpigapicha Wetu
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Daniel Mushi.

Serikali imesema kuwa ni muhimu kuwajengea vijana wa Afrika uwezo wa stadi za kazi ili waweze kujiajiri, kuanzisha kampuni zao na kuajiri wengine, kutokana na ukweli kuwa Bara la Afrika lina idadi kubwa ya vijana, hivyo ni bara changa lenye nguvu kazi kubwa.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Daniel Mushi, wakati akimwakilisha Waziri wa Elimu, Prof. Adolf Mkenda, katika kongamano la kimataifa linalojadili masuala ya mafunzo ya ufundi na ufundi stadi.

Kongamano hilo limewakutanisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, likiandaliwa kwa ushirikiano na Umoja wa Waajiri Tanzania (ATE), Chama cha Wafanyakazi Tanzania na vyama vinavyofanana kutoka nchini Denmark.

Katika hotuba yake, Mushi amesisitiza kuwa hivi karibuni Rais Samia alizindua Sera mpya ya Elimu na Mafunzo, ambayo imeweka kipaumbele kikubwa kwenye mafunzo ya amali, yaani mafunzo kwa vitendo, ufundi na ufundi stadi kwa ujumla.

Ameeleza kuwa juhudi hizo zinalenga kuhakikisha vijana wanapewa ujuzi utakaowawezesha kujitegemea kwa kujiajiri na hata kuwaajiri wengine, jambo ambalo litasaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana nchini.

“Mchakato huu wa kutengeneza mitaala kupitia majukwaa kama haya ni muhimu sana kwa sababu unatupatia mrejesho kutoka kwa waajiri juu ya aina ya stadi wanazozitaka kwa vijana. Hii inatuwezesha kama serikali kushirikiana kwa karibu na soko la ajira ili kuhakikisha mafunzo yanayoendeshwa yanakidhi mahitaji ya wakati huu,” amesema Mushi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzanne Ndomba, amesema kuwa baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi wa kukuza ujuzi mwaka jana, wamebahatika kupata nafasi nyingine ya kuendeleza mradi huo kwa lengo la kuimarisha soko la ajira nchini.

Amesema kuwa kupitia mradi huo, ATE imeanzisha mabaraza ya kukuza ujuzi katika sekta tatu kuu ambazo ni sekta ya madini, ukarimu na utalii pamoja na viwanda. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa waajiri na serikali wanaendelea kushirikiana katika kukabiliana na changamoto ya ajira, hasa kwa vijana.

“Tumekuwa tukizungumzia siyo tu suala la ujuzi, bali pia kuhakikisha kuwa vijana wanapata kazi, na kazi hizo ziwe ni kazi zenye staha,” amesema Ndomba.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), Leodgar Tenga, amesema kuwa viwanda ni nguzo muhimu ya maendeleo ya Taifa, huku akisisitiza kuwa ufanisi wa sekta hiyo unategemea kwa kiasi kikubwa uwezo wa wafanyakazi waliopo viwandani.

Tenga amepongeza juhudi zinazofanywa na ATE katika kuhakikisha viwanda nchini vinapata wafanyakazi wenye ujuzi, maarifa na ubora unaohitajika katika uzalishaji.

“ATE wanafanya kazi kubwa sana katika kuhakikisha tunaendelea kupata wafanyakazi bora kwa ajili ya viwanda vyetu. Tunatambua mchango wao na tunaupongeza sana,” amesema Tenga.

Aidha, ameongeza kuwa wataendelea kushirikiana kwa karibu na ATE katika juhudi za kuendeleza ajira kwa vijana na kuongeza tija katika sekta ya viwanda nchini.

“Tutazidi kuwa karibu na ATE ili kuhakikisha vijana wanapata ajira na viwanda vinaongeza ufanisi kupitia nguvu kazi yenye weledi,” amesisitiza.