SIKU YA KUTOKOMEZA FISTULA DUNIANI; Unyanyapaa ulivyo kikwazo

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 10:25 AM May 23 2025
Mwandishi wa habari wa habari hii, akizungumza na Frida Jason
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwandishi wa habari wa habari hii, akizungumza na Frida Jason

UNYANYAPAA kwenye jamii, athari kisaikolojia kwa wanaougua fistula, kasoro katika upasuaji ni miongoni mwa changamoto zilizomo kwenye ugonjwa huo, wakati leo ikiadhimishwa Siku ya Kimataifa Kutokomeza Fistula Duniani.

Baadhi ya wagonjwa wanaougua na bado hawajapata elimu, huathirika kiafya kwa namna ya pili, kwa kuwa hujizuia kunywa maji na kuwafanya haja ndogo wanayojisaidia kuwa na viwango vikubwa vya chumvi, na kusababisha vidonda na michubuko.

Kadhalika, kutokana na kuepuka adha ya kutokwa haja ndogo kila mara, baadhi ya wanaougua hupata athari ya pili kiafya kwa kuwa hujizuia kunywa maji, ikisababisha kupata michubuko na vidonda sehemu za siri.

Bingwa wa Magonjwa ya Kinamama na Mfumo wa Uzazi kutoka hospitali ya CCBRT, Dk. Peter Majinge, anasema: Kuna unyanyapaa. Kinamama ambao wanaugua wanatengwa na wapendwa wao ndani ya familia na nje ya jamii. Nakumbuka kuna baadhi ya akinamama walieleza walifikia hatua ya kutaka kujiua, wametengwa na waume, wanafikia hatua ya kujidhuru kimaisha.”

Frida Jason (si jina lake halisi), aligundulika kuwa ana fistula. Akiwa wodini siku 13 baada ya kufanyiwa upasuaji, akizungumza na gazeti hili alisema kwamba ameugua kwa takribani miaka 20, tangu mwaka 2006 kutokana na uzazi.

“Maendeleo naona mazuri, ni siku ya 13 tangu upasuaji. Kati ya watu waliokaa sana na huu ugonjwa ni mimi, tangu 2006. Nilitibiwa awali lakini sikuwa na fedha, nikasema ngoja nitulie na watoto walikuwa wadogo.

“Huu ni ugonjwa wa aibu, unashinda unajifunikafunika. Hutaki watu wajue. Kumbe unavyojifungia ndio mbaya. Ukitaka kutoka hadi ujistiri uvae, ili usiadhirike," anasema Frida.