TAKUKURU: Sekta ya Ardhi kinara malalamiko ya rushwa Dodoma

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 12:16 PM May 09 2025
Mkuu wa Takukuru mkoa wa Dodoma Christopher Myava,akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma,kuhusu taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu.
RENATHA MSUNGU
Mkuu wa Takukuru mkoa wa Dodoma Christopher Myava,akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma,kuhusu taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Dodoma, imeitaja sekta ya ardhi kuwa kinara wa malalamiko yenye viashiria vya rushwa, ikiongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya mashitaka kutoka kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma, Christopher Myava, Mei 8, 2025, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo kwa robo ya tatu ya mwaka, kuanzia Januari hadi Machi.

Myava alisema kuwa sekta ya ardhi inaongoza kwa kuwa na malalamiko 47 yenye viashiria vya rushwa, ikifuatiwa na sekta ya elimu (malalamiko 18), Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) yenye malalamiko 15, na jeshi la polisi likiwa na malalamiko 10.

Sekta nyingine zenye malalamiko ni pamoja na sekta binafsi (malalamiko 8), kilimo (6), utawala, maji na afya (malalamiko 5 kila moja), mifugo, mahakama, fedha na serikali kuu (malalamiko 4 kila sekta).

Aidha, Myava alitumia fursa hiyo kuwakumbusha na kuwataka wagombea wa nafasi mbalimbali kuelekea Uchaguzi Mkuu kuepuka kujihusisha na vitendo vya rushwa, ikiwa ni pamoja na kuwarubuni wananchi kwa ahadi au zawadi ili wawachague. Alisisitiza kuwa wagombea wanapaswa kufuata taratibu za uchaguzi kama zinavyoelekezwa na vyombo husika.

Katika hatua nyingine, TAKUKURU mkoa wa Dodoma imesema imefuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 50, ambapo katika miradi 32 iliyohusisha sekta ya afya, ujenzi wa barabara na elimu, imefanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi milioni 13.