TANESCO kufanya maboresho ya Luku Dar, Pwani

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 06:32 PM Jul 15 2024
 Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa Umma TANESCO, Irene Gowelle.
Picha: Maulid Mmbaga
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa Umma TANESCO, Irene Gowelle.

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) linatarajia ifikapo Julai 24, mwaka huu kuanza zoezi la kufanya maboresho ya mfumo wa Luku katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Hayo yamebainishwa leo mkoani Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa Umma TANESCO, Irene Gowelle, amesema lengo kuu la kufanya maboresho hayo ni ili kuendana na mabadiliko ya kimfumo ya viwango vya mita za Luku vya kimataifa.
 
Pia ameshauri wale wenye utaratibu wa kununua umeme na kuutunza, kwamba kabla hawajafanyiwa maboresho waingize kwanza umeme wao na watakapohakikisha kuwa umeshaingia ndipo waingize tokeni za maboresho ya mfumo wa Luku.
 
“Tunasisitiza hilo kwasababu kutokufanya hivyo kutasababisha mteja kupoteza umeme wake iwapo ataanza kuingiza tokeni za maboresho ya mfumo wa Luku kabla ya umeme wake wa zamani. Maboresho haya pia ni kwaajili ya kuongeza ufanisi na usalama wa mita,” amesema Irene.
 
Aidha, alisisitiza watanzania kutoa ushirikiano katika kufanikisha zoezi hilo, huku akitahadharisha kwamba kwa wale ambao hawatafanya maboresho ya mita zao baada ya Novemba 24, mwaka huu hawatapata huduma ya umeme.
 
Ameeleza kuwa maboresho hayo yatakapoanza mteja baada ya kununua umeme atapokea makundi matatu yenye jumla ya tarakimu 60, na kwamba kila kundi litakuwa na tarakimu 20 na mawili ya mwanzo ni kwa ajili ya maboresho na la mwisho litakuwa ni umeme ambao atakuwa amenunua.
 
Amesema mteja ataingiza makundi yote ya tarakimu kwa kufuata mpangilio kama utakavyokuwa unasomeka kwenye risiti ya malipo, baada ya hapo atakuwa amekamilisha kufanya maboresho na kuingiza umeme wake alionunua.
 
Pia amesema kwa wale watakaokutana na changamoto yoyote wakati wa zoezi hilo wapige TANESCO huduma kwa wateja ili wapatiwe msaada, kwa namba ambazo ni Temeke 0694169798, Kinondoni Kusini 0756251753, Ilala 0733212575, Kinondoni Kaskazini 0692768587, Pwani 0738256237.