Timu ya madaktari kutoka China watibu Watanzania milioni 10

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 08:29 PM Jul 15 2024

Kiongozi wa Timu ya Madaktari 27 wa China, Zhang Jungiao (kulia) na Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo Liu Yimin, (kushoto) wakizungumza na waandishi wa habari mafanikio yaliyopatikana tangu awamu ya kwanza ya madaktari hao ilipowasili nchini mwaka 1964.
Picha:Frank Monyo
Kiongozi wa Timu ya Madaktari 27 wa China, Zhang Jungiao (kulia) na Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo Liu Yimin, (kushoto) wakizungumza na waandishi wa habari mafanikio yaliyopatikana tangu awamu ya kwanza ya madaktari hao ilipowasili nchini mwaka 1964.

JUMLA ya watu milioni 10 wamenufaika na huduma za matibabu zinazotolewa na timu ya madaktari kutoka China katika kipindi cha miaka 60 iliyopita.

Kiongozi wa timu ya madaktari 27 wa China, Dk. Zhang Jungiao,ameyasema hayo leo  Jijini Dar es Salaam wakati akielezea mafanikio yaliyopatikana tangu kundi la kwanza lilipowasili nchini mwaka 1964.

Amesema kuwa timu ya matibabu ni pamoja na upasuaji wa moyo, matibabu ya wagonjwa mahututi, dawa ya usingizi, watoto, mifupa na upasuaji wa neva.

Dk. Jungiao amesema katika ushirikiano huo timu ya madaktari hao ilitoa uzoefu wao pamoja na kutoa mafunzo kwa madaktari wa Tanzania jinsi ya kutumia vifaa vipya vya kisasa kutoa huduma bora za afya.

"Tulifanya jitihada za makusudi ili kuziba pengo hilo kwa kubadilishana ujuzi kwa madaktari na wauguzi wa ndani (Tanzania) ili kuokoa maisha ya Watanzania kwa kuhakikisha utoaji wa huduma za afya za hali ya juu na za kiwango zinatolewa," amesema.

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo, Liu Yimin, kutoka timu hiyo ametoa wito kwa Watanzania kufanya uchunguzi wa mara kwa mara wa afya zao ili kugundua ugonjwa kwa wakati na kupata matibabu.

Amesema timu hiyo imegundua wagonjwa wengi wanaliowapatia matibabu, wamechelewa kuchukua hatua ya kufanya uchunguzi wa magonjwa ambapo wengi wao yamesababisha vifo.

1

"Magonjwa madogo madogo yamekuwa tatizo kubwa, na pia watu wengi wana magonjwa ya kuzaliwa au urithi ambayo yanahitaji kuonana na daktari mara moja.

Dk. Yimin pia amewataka Watanzania kuwa na utamaduni wa kula mlo kamili na kubadili mfumo wa maisha ili kuzuia ongezeko la watu wanaoripotiwa kuugua magonjwa yasiyoambukiza (NCD).

“NCDs zinaongezeka nchini Tanzania. Kwa hivyo, ni lazima tuepuke maisha yasiyofaa kama watu binafsi au familia ili kujiepusha na magonjwa,” amesema.
2

Amefafanua kuwa China ugonjwa wa moyo na mishipa ugunduliwa zaidi kwa watu wenye umri wa miaka 70 hadi 80 wakati Tanzania ugonjwa huo unapatikana sana vijana wenye umri wa miaka 25 hadi 35.

Hata hivyo Dk. Yimin ameipongeza Serikali ya China na Tanzania kwa mpango wa kuanzisha taasisi ya magonjwa ya moyo nchini na kuongeza kuwa imekuwa kituo kikubwa na cha juu zaidi cha uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo Tanzania, na hata Afrika Mashariki.

3