Vijana wapewe fursa ya kusikika, kufanya maamuzi

By Mary Geofrey , Nipashe
Published at 07:00 PM Jul 15 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la Liberty Sparks, Evans Exaud
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la Liberty Sparks, Evans Exaud

IMEELEZWA kuwa vijana wana nafasi kubwa ya kufanya mabadiliko kwenye jamii zao kama wakipewa fursa ya kusikika, kuongea na kufanya wanachoamini.

Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la Liberty Sparks, Evans Exaud, katika mkutano maalum uliyowakutanisha vijana kutoka vyuo mbalimbali.

Lengo ni kujadiliana na kujifunza ni kwa jinsi gani wanaweza kuanzisha cheche za mabadiliko kwa kuweka ubunifu unaoweza kuisaidia jamii kwenye ukuaji wa uchumi.

Exaud amesema asilimia 50 ya watu waliopo nchini ni vijana na wengi wamepata elimu kutoka maeneo mbalimbali, endapo wakishirikishwa ipasavyo wanaweza kufanya mambo makubwa ya kimaendeleo hasa kwenye masuala ya biashara ambazo zimejikita kuleta mabadiliko nchini.

“Vijana wanatakiwa kupewa nafasi, kutengenezewa mazingira rafiki ambayo yatawawezesha kufanya biashara hasa katika maeneo ya mipakani na mijini ili kuweza kuchangia maendeleo ya kiuchumi katika nchi yetu,” amesema Exaud

Awali akifungua mkutano huo kwa niaba ya Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu(Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Patrobas Katambi, Mkurugenzi Ukuzaji Tija kutoka wizara hiyo, Yohana Madadi alisema serikali inatambua kuwa vijana ni nguvu kazi muhimu katika taifa na kwamba wanategemewa hasa kwenye kuleta mabadiliko na maendeleo nchini.

1

Amesema serikali ya awamu ya sita imejidhatiti katika kuhakikisha kuwa vijana wanapata fusra za kutosha, kujifunza pamoja na kuonesha uwezo wao kwenye nyanja mbalimbali.

Aidha, amesema wizara imeboresha mwongozo wa utoaji mikopo kupitia mfuko wa maendeleo ambapo zaidi ya vijana 392 na miradi 156 imefadhiliwa kupitia mfuko huku zaidi ya Sh. Bilioni 8 zimetolewa ili kufanikisha miradi hiyo ya vijana.

Amesema wizara pia imeanzisha program ya ukuzaji ujuzi ambapo vijana 134,093 wamenufaika kupitia uwanagenzi huku vijana 20,330 wamepatiwa mafunzo ya kurasimisha ujuzi na 19,190 wamepatiwa mafunzo ya uzoefu kazini.

Naye Yumilit Franck mwanafunzi wa mwaka wa pili kutoka katika chuo kimoja wapo huko nchini Marekani alisema amekuja katika mkutano huo ili kuweza kujifunza na kuongeza ujuzi kwa kusikia kutoka kwa watu wenye ufanisi kwenye kazi zao.
2