Wachimbaji wadogo wa kokoto katika Halmashauri ya Mji wa Njombe wameiomba Serikali ya mkoa kuhakikisha miradi ya ujenzi inatumia malighafi zinazozalishwa na wachimbaji wa ndani ili kuwawezesha kiuchumi.
Ombi hilo limetolewa na wachimbaji wa kokoto wa mtaa wa Buguruni, wanaofanya shughuli katika jiwe la Ganga Lyandefu, walipowasilisha kero zao kwa Mbunge wa Viti Maalumu wa Mkoa wa Njombe kupitia CHAUMMA, Sigrada Mligo, alipofanya ziara ya kusikiliza changamoto zinazowakabili.
Mmoja wa wachimbaji hao, Lucas Petro, amesema pamoja na Mkoa wa Njombe kutekeleza miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa tawi la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), bado hawapati nafasi ya kutoa malighafi zao katika miradi hiyo, jambo linalowanyima fursa ya kukuza kipato.
Kwa upande wake, Mbunge Sigrada Mligo ameahidi kufuatilia suala hilo na kusimamia upunguzaji wa tozo na ushuru, ili kuhakikisha wachimbaji hao wanapata mazingira wezeshi ya kuuza malighafi wanazozalisha.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED