Wakili Muga asema kipaumbele chake kudhibiti ufujaji wa fedha TLS

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 08:32 PM Jul 15 2024
Mgombea urais wa Chama cha Wanasheria (TLS), Emmanuel Muga akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusiana na vipaumbele vyake iwapo atachaguliwa kuwa rais, cha kwanza ni kudhibiti ada za wananchama.
Picha: Grace Gurisha
Mgombea urais wa Chama cha Wanasheria (TLS), Emmanuel Muga akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusiana na vipaumbele vyake iwapo atachaguliwa kuwa rais, cha kwanza ni kudhibiti ada za wananchama.

MGOMBEA urais wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS), Emmanuel Muga amesema kipaumbele chake cha kwanza ni udhibiti ufujaji wa fedha za chama, kwa sababu wanachama wanaongezeka kila mwaka lakini viongozi wanasema fedha hakuna.

Aidha, amesema siku 30 za mwanzo wa utawala wake atahakikisha wanaweka mfumo wa fedha mudhubuti unaotumia teknolojia, fedha ikilipwa inaonekana na nikitolewa pia inaonekana.

Muga amesema hayo leo, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na vipaumbele vyake iwapo atachaguliwa kwenye nafasi hiyo, akisisitiza atahakikisha fedha (ada) za wanachama zinaleta mabadiliko katika chama hicho.

Amesema kuwa hivi sasa wanachama wanamalalamiko mengi kuhusiana na fedha zinavyotumika hivyo ataweka mifumo ya kuhakikisha hakuna ufujaji wa fedha na huo ndiyo utakuwa mwisho wa matumizi mabaya ya fedha za wananchama.

Muga, ambaye alikuwa aliwahi kuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam kati ya mwaka 2019-2021 ambapo kwa kipindi hicho aliweza kuwaunganisha wanachama kuwa kitu kimoja,  akiwa rais atafanya mambo makubwa zaidi ya waliyoyafanya kwa kipindi hicho.

Amesema udhibiti wa fedha utakuwa kati ya vipaumbele vyake vya muda mfupi ambavyo pia vitahusisha kuleta umoja miongoni mwa mawakili, kusimamia nidhamu za mawakili na kulinda hadhii na taswira faini ya sheria.

Pia, amesema kamati zao zenyewe ndio zitakazoshughulikia masuala vya maadili ya mawakili, hawatasubiri mawakili wahukumiwe na kamati ya mawakili inayoongozwa na Jaji Ntemi Kilekamajenga.

Pia, amesema atakuwa na mpango mkakati wa miaka mitano unaoakisi kazi na malengo ya TLS kama yalivyokwenye sheria, mpango huo utaangalia jamii ya watanzania katika masuala ya sheria na namna nzuri ya kutimiza wajibu wake kwa mahakama.