Miili ya wanandoa, Geofrey Anael Mota (60) na Blandina Felix Ngowi (53), waliofariki dunia kwa wakati mmoja katika tukio la kustaajabisha, lililotokea Mtaa wa Msufini, Kata ya Msaranga, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, itazikwa kesho shambani kwake eneo la Kariwa Chini-Rau.
Mtoto wa marehemu, Abraham Mota, akizungumza leo Juni 3, 2025 na Nipashe Digital, amesema ukoo wa Mota umepanga wazazi wake watazikwa Juni 4 mwaka huu.
Wanandoa hao, Geofrey Mota na Blandina Ngowi (53), walipoteza maisha Mei 29 mwaka huu, majira ya saa 1:30 usiku; wakiwa nyumbani kwao Mtaa wa Msufini, baada ya baba kuuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni, huku mama mwili wake ukiwa haujakutwa na majeraha.
“Ibada ya kuaga wanandoa hao itafanyika kesho katika Kanisa la Usharika wa Msaranga-Mandaka Centre, Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT); na baadae tutaenda kuwapumzisha kwenye eneo la familia lililoko Kata ya Rau, Mtaa wa Kariwa Chini.
…Tumeruhusiwa na Polisi kuzika, wamesema ripoti ya uchunguzi inaonyesha mama alifariki kutokana na depression (sonona), kwa kile alichokishuhudia kwa mumewe akiuawa.”
Mei 30 mwaka huu, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP), Simon Maigwa, alisema jeshi hilo linawasaka watu waliohusika katika mauaji hayo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED