Watoto wametakiwa kutokuoga wala kujisafisha mara baada ya kufanyiwa ukatili wa kingono ili kuepusha kuondoa ushahidi muhimu unaoweza kusaidia kubaini wahalifu na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
Wito huo umetolewa na Mtandao wa Polisi Wanawake wa Mkoa wa Geita walipotembelea Kituo cha Watoto Wanaoishi katika Mazingira Magumu cha Bright Light, ambapo wametoa msaada wa vyakula, sabuni na taulo za kike kwa watoto 53.
Mtandao wa Polisi Wanawake umetoa msaada huo kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, inayotarajiwa kufanyika Machi 8, 2025, jijini Arusha.
Akizungumza katika tukio hilo, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Geita, Christina Katana, amesema moja ya changamoto kubwa katika kesi za ukatili wa kijinsia ni waathirika kuharibu ushahidi kwa kuoga au kubadili nguo kabla ya kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu.
"Mtoto akifanyiwa ukatili wa kingono, ni muhimu kuripoti haraka kwa mamlaka husika au kwa mtu anayeaminika bila kuoga au kubadili nguo. Hii husaidia wataalamu wa afya na vyombo vya sheria kupata ushahidi wa kitabibu na kisheria ili kuwachukulia hatua wahusika," amesema Katana.
Mbali na kutoa msaada, mtandao huo ulitoa elimu kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia, jinsi ya kujilinda, na umuhimu wa kuwa wawazi kwa walimu, wazazi, au ndugu wengine badala ya kunyamazia unyanyasaji wanaokutana nao.
Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa ukatili dhidi ya watoto bado ni tatizo kubwa nchini, ukiwa na athari za muda mfupi na mrefu kwa waathirika. Tafiti zinaeleza kuwa watoto waliokumbwa na ukatili wa kijinsia hukumbana na matatizo ya kisaikolojia, hofu, msongo wa mawazo, na wakati mwingine kushindwa kuendelea na masomo yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Watoto Wanaoishi kwenye Mazingira Magumu cha Bright Light, Methew Daniel, amesema kituo hicho kinalea na kusomesha watoto 53. Aliongeza kuwa wanapowachukua watoto kutoka mazingira hatarishi, huwapatia elimu ya saikolojia ili kuwasaidia kurejea katika hali ya kawaida na kuishi maisha bora badala ya kuhisi kuwa maisha ya mtaani ndiyo suluhisho sahihi kwao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED