Waziri wa Maji wa Tanzania, Jumaa Aweso, kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Audrey Azoulay, wamezindua rasmi Mradi wa Usimamizi na Uendelezaji wa Rasilimali za Maji yaliyo chini ya ardhi katika Mlima Kilimanjaro.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika leo, Waziri Aweso ameeleza kuwa mradi huo utaanza kutekelezwa rasmi Januari 2026, na utalenga kufanya tafiti za kina kuhusu maji yaliyo chini ya ardhi ili kuhakikisha yanaweza kukidhi mahitaji ya watu na kusaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Alisisitiza kuwa mabadiliko ya tabianchi yamekuwa na athari kubwa kwenye vyanzo vya maji, ikiwa ni pamoja na kukauka kwa mito na chemchem, na kwamba mradi huu utasaidia kupambana na changamoto hizo.
Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Audrey Azoulay, amesema kuwa hatua ya sasa ni kuchora ramani ya maeneo yenye vyanzo vya maji vya kutosha katika wilaya za Hai na Rombo mkoani Kilimanjaro. Azoulay alisisitiza kuwa mradi huu ni sehemu ya juhudi za kimataifa za kuhakikisha usimamizi endelevu wa rasilimali za maji na kwamba, kupitia ushirikiano na Tanzania, UNESCO inajitahidi kuhakikisha maendeleo endelevu ya sekta ya maji.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji wa Kenya, Mhandisi Eric Mugaa, amesema mradi huu utawanufaisha zaidi ya milioni mbili za wananchi kutoka nchi zote mbili. Mhandisi Mugaa alieleza kuwa mradi huo utaongeza ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya na kuwa msaada mkubwa katika kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji. Amesema pia kuwa utasaidia sekta ya kilimo cha umwagiliaji na kutoa huduma muhimu za kijamii katika maeneo yanayozunguka Mlima Kilimanjaro.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Tanzania, Prof. Adolph Mkenda, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Rombo, amesisitiza kuwa mradi huu utasaidia wananchi wa Rombo na maeneo jirani kupata maji safi na salama kwa uhakika.
Mradi huu ni sehemu ya juhudi za pamoja za kuimarisha upatikanaji wa maji safi na kulinda vyanzo vya maji katika ukanda wa Mlima Kilimanjaro, kuhakikisha rasilimali hii muhimu inatunzwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED