MSEGI Nyakilang’anyi (48), Mkazi wa Mtaa wa Kibaoni katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Hai, mkoani Kilimanjaro, aliyepata ulemavu wa viungo kwa ajali ya kuanguka barabarani miaka 24 iliyopita,amesema anatamani kuachana na kazi ya kuombaomba mitaani, kwa sababu anavyo viungo vizuri vya kufanya kazi.
Nyakilang’anyi, ambaye ni baba wa watoto watatu, amesema hivi sasa anatafakari kazi ya atakayoifanya ili imwezeshe kuingiza kipato halali na kuachana na kazi hiyo, baada ya mdau wa maendeleo wilayani humo, Shaban Mwanga, kuguswa na changamoto yake ya maisha, ikiwamo kukosa kiti mwendo.
Nyakilang’anyi, anayezunguka barabarani na mitaa mbalimbali ya Wilaya ya Hai kutafuta riziki, akisaidiwa na mkewe, ameiambia Nipashe Digital leo Machi 6, 2025, kuwa amemsikia Shaban Mwanga, akisaidia watu wengi, na ndipo na yeye alikopata nguvu ya kumtafuta mdau huyo ili aweze kupata msaada kwake.
“Mungu ambariki sana Shaban Mwanga, najua ananisikia kwa huruma zake, naomba anisaidie kile cha kunisaidia, aniwezeshe na mimi na familia yangu tutapata riziki. Namshukuru sana, kwa sababu ameahidi kuniletea baiskeli ya matairi matatu. Nimemuomba akasema atatua changamoto yangu kwa kunisaidia baiskeli.
…Huko baadae, nitamuombea Mungu, ili arudi aguswe zaidi aweze kunisaidia Bajaj (pikipiki ya matairi matatu), ili niweze kuwa napata kipato kitakachoinua maisha yangu, kuliko niendelee kuomba barabarani.
Ndugu zangu, kuomba barabarani mimi sitaki, kwa sababu mimi nina viungo vizuri kabisa vya kufanya kazi.”
Alipotafutwa na Nipashe Digital kwa njia ya simu, Shaban Mwanga, amesema, “Ni kweli nimepokea video (picha mjongeo) ya moja ya mlemavu kutoka Wilaya ya Hai, ambaye ameonyesha awali amekwenda kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, na kupewa kibali cha kuomba msaada kutokana na tatizo lake la baiskeli ya miguu mitatu, ambayo ndiyo humsaidia kutafuta riziki, na ndiyo mguu wake, ambao huutumia kutokana na ulemavu wake wa mguu.
…Nimepokea kwa huzuni sana taarifa hii, kwa jinsi anavyoteseka; kwa kuwa nae ni mwanadamu na anatakiwa kuishi kama watu wengine. Hatuna budi kwa namna moja au nyingine kuhakikisha kwamba kama sadaka tunawasaidia watu hawa.”
Aidha, mdau huyo wa maendeleo, amesema tayari amemwagiza mmoja wa maofisa wake aliyeko kanda ya kaskazini, kwenda kumuona mlemavu huyo na kumpa taarifa ya aina gani ya baiskeli, ambayo anaihitaji ili aweze kumpatia.
Zaidi Mwanga aliongeza: “Nitampa baiskeli hiyo, ili aweze kuendelea na maisha yake ya kawaida ya kujitafutia riziki, lakini na maisha mengine. Sisi lengo letu kubwa ni kuhakikisha tunaleta furaha katika familia, tunaleta furaha katika jamii; japo ni kidogo lakini kidogo hicho tunakitoa, kinaleta furaha lakini kinaleta amani ndani ya mioyo ya wale wahitaji.
…Ifahamike kwamba kama awali nilivyosema, kweli Dk. Samia Suluhu Hassan, anafanya anafanya mambo makubwa, lakini sisi wana jamii, sisi wadau wa maendeleo; lengo letu ni kuangalia yale mambo ambayo siyo lazima yamfikie Rais wetu, sisi tutayafanya.”
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED