Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini, Selina Koka, ametoa msaada wa sabuni kwa wodi ya wazazi katika Hospitali ya Wilaya ya Lulanzi, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayofikia kilele chake Machi 8.
Selina, akiwa ameongozana na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini, amekabidhi msaada huo kwa uongozi wa hospitali hiyo huku akiahidi kupeleka makoti 15 kwa madaktari pamoja na mashuka kwa ajili ya wodi mbalimbali hospitalini hapo.
Aidha, alibainisha kuwa atarejea hospitalini hapo kwa ajili ya kupanda miti ya kivuli, ikiwa ni jitihada za kulinda mazingira na kuhakikisha wananchi wanapata sehemu za kupumzikia wanapofika hospitalini.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Lulanzi, Dk. Betha Makidika, amemshukuru Selina Koka kwa msaada wake na namna ambavyo amekuwa akijitoa kusaidia hospitali hiyo mara kwa mara.
"Wanawake waliopo wodini wanapopata watu wa kuwafariji wanajisikia vizuri. Jambo mlilofanya leo ni faraja kubwa kwetu. Mama Koka amekuwa mstari wa mbele katika kusaidia hospitali hii kwa njia mbalimbali, na tunaishukuru sana kwa moyo wake wa kujali," alisema Dk. Makidika.
Ameongeza kuwa serikali tayari imetoa vifaa vyote muhimu kwa hospitali hiyo, na jukumu lililopo kwa sasa ni kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED