Bonde la Wami/Ruvu Pwani yafariji watoto waliolazwa Muhimbili

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:44 PM Mar 06 2025
news
Picha: Mpigapicha Wetu
Bonde la Wami/Ruvu Pwani yafariji watoto waliolazwa Muhimbili.

Wanawake wa Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu kidakio cha Pwani wametoa msaada wa vitu mbalimbali kwa wazazi wa watoto waliolazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Msaada huo ni katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ambapo Kitaifa yanatarajiwa kufanyika mkoani Arusha Machi 8, 2025.  

Afisa Maendeleo ya Jamii wa bonde hilo, Flora Muro, ambaye alimwakilisha Afisa wa Kidakio, Mhandisi Diana Kimbute, amesema lengo la ziara hiyo ni kuwafariji watoto wachanga waliolazwa katika wodi namba 36 na 37 kutokana na matatizo mbalimbali ya kiafya.

Amesema bodi hiyo inasisitiza umuhimu wa mshikamano wa jamii, upendo, na kusaidiana, hasa kwa watu wenye uhitaji, ikiwa ni sehemu ya uwajibikaji wa kijamii.

Amesema kupitia ziara hio, bodi inahimiza jamii kuwa na moyo wa huruma kwa wagonjwa na watu wenye mahitaji maalum, huku ikikumbusha kuwa kusaidia wengine ni tendo la ibada lenye mchango mkubwa katika kujenga jamii yenye mshikamano na upendo.

“Tunamshukuru sana Mkurugenzi (Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu Mhandisi Elibariki Mmasi) kwa kuwezesha safari hii muhimu, ambayo inalenga kuonyesha mshikamano na upendo kwa watoto hawa wadogo,” ilielezwa katika ziara hiyo.

Meneja wa Jengo la Wazazi katika hospitali hiyo, Christina Mwandalima, ameishukuru bodi hiyo kwa upendo waliouonesha kwa watoto hao, akisema: 

“Ziara hii imetupa matumaini na kutufanya tusihisi kuwa pekee katika safari hii ya afya. Pia, inatuhamasisha kuona umuhimu wa kusaidiana na kujali ustawi wa jamii nzima.”