Polisi yaonya wanaotaka kuvuruga amani kipindi cha uchaguzi

By Ida Mushi , Nipashe
Published at 07:21 PM Mar 06 2025
CPA, Awadhi Juma
PICHA: MTANDAO
CPA, Awadhi Juma

KAMISHNA wa Jeshi la Polisi anayeshughulikia kamisheni ya operesheni na mafunzo CPA, Awadhi Juma amewaondoa hofu wananchi kuwa jeshi hilo litaendelea kuhakikisha usalama, amani na utulivu vinaendelea kuimarishwa sasa, wakati na baada ya uchaguzi na kamwe hawatakuwa na muhali na mtu yeyote atakayejaribu kuharibu uchaguzi.

Kamishna Awadhi alisema hayo wakati akihitimisha mafunzo ya miezi mitatu kwa askari 1,074 juu ya uongozi mdogo wa ngazi ya Sajini taji (sajenti na staff sajenti) katika chuo cha maofisa wa Polisi Tanzania cha Kidatu, kilichopo wilayani  Kilombero Mkoani Morogoro.

Akasema kwa sasa hali ya nchi ni shwari, tulivu na usalama umeendelea kutamalaki kwa sababu Jeshi hilo lipo na kwamba wataendelea kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha hali hiyo inaendelea kuwepo sambamba na kutoa wito kwa wananchi kuwafichua watu wachache watakaojaribu kuhatarisha amani na usalama wa nchi.

"Tumejipanga vizuri kwenye hili,tutashughulika na watu wa hovyo hovyo wanaodhani wanaweza kufanya vinginevyo, blabla (maneno maneno) mnazozisikia zisiwanyime usingizi,uchaguzi utafanyika kwa amani na utulivu mkubwa" alisema kiongozi huyo mwenye dhamana ya operesheni na mafunzo kwa Jeshi la Polisi.

Aidha akamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaboreshea askari mafunzo ya mara kwa mara, kutoa vitendea kazi na vifaa vingine hivyo Poliisi wana deni kubwa kwa Serikali ya awamu ya Sita kwa kuhakikisha Ulinzi, usalama na amani ya nchi vinazingatiwa.

"Tuna uwezo wa kushughulika kwa namna yeyote na mhalifu yeyote,tutawashughulikia vizuri tu wale wote watakaochomoza sharubu zao kuchochea uhalifu, sisi tunazingatia 4R za Rais, sasa watakaoshindwa Sheria itachukua mkondo wake"-alisisitiza.

Mapema Mkuu wa chuo cha Polisi Kidatu, Kamishna Msaidizi mwandamizi wa Polisi, SACP Zarau Hassan Mpangule licha ya kuiomba Serikali kuboresha upatikanaji wa mawasiliano hasa ya kutuma fedha kutoka TTCL kwenda mitandao mingine kutokana na huduma hiyo kutoweka kwa muda mrefu, huku chuo hicho kikiwa hakina mawasiliano mengine zaidi ya TTCL, akapongeza hatua ya Serikali kuja na mpango wa mafunzo ambao umewezesha askari wengi kupanda vyeo .

"Zamani kwa askari kupanda vyeo ilikuwa ni shughuli, wengi walistaafu wakiwa na vyeo vya chini, lakini sasa askari wengi wanapata fursa za mafunzo kusomea vyeo tofauti na zamani, lakini kuna fursa za mafunzo mengi ya nje ya nchi hata hapa Kidatu kwa siku za karibuni askari watano wamepata mafunzo toka nchi mbalimbali na watatu bado wako Urusi kwa kozi ya muda mrefu"-alisema Mkuu huyo wa chuo cha maofisa wa Polisi Kidatu.

Aidha akasema askari hao wahitimu wamepata mafunzo mbalimbali ya nadharia na vitendo, na pia namna mbalimbali ya kukabiliana na uhalifu ikiwemo wizi wa kimtandao.

Pamoja na kushukuru kwa jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali kwa Polisi ikiwemo ujenzi wa jengo la utawala chuoni hapo ambalo limeshaanza kujengwa na kukamilika kwake kutagharimu zaidi ya bilioni 1.6, akaomba jitihada zaidi kufanywa kuboresha miundombinu katika chuo hicho ikiwemo ujenzi wa nyumba za watumishi na mambo mengine.

Baadhi ya wadau waliohudhuria akiwemo Mstahiki Meya mstaafu wa Manispaa ya Morogoro, Amir Juma Nondo, akasema ni vyema Watanzania wakachukua tahadhari kwa kuacha kufanya yale yatakayochochea kuharibu uchaguzi.

"Na mtu asikubali kutumika kuanzisha choko choko, kwasababu akipata madhara ni yake na familia yake na sio taifa, tuepuke sana kuleta vurugu ama ghasia zozote wakati huu wa kabla, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi" alisisitiza Nondo.