Serikali kujenga mtandao mkubwa wa mabomba ya gesi- Dk. Biteko

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:16 PM Mar 06 2025
Serikali kujenga mtandao mkubwa wa mabomba ya gesi- Dk. Biteko.
Picha:Mpigapicha Wetu
Serikali kujenga mtandao mkubwa wa mabomba ya gesi- Dk. Biteko.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Rashal Energies, Farhiya Warsame ambayo inajenga Bomba la Gesi kutoka Kisemvule hadi Mbagala jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matumizi ya vituo vya Kujazia Gesi kwenye Magari (CNG) na kwenye viwanda.

Mazungumzo hayo yamefanyika jijini Dar es Salaam tarehe 06 Machi, 2025 kando ya Kongamano na Maonesho ya Petroli ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAPCE’25) linalofanyika kwa  Siku Tatu jijini Dar es Salaam.

Dk.Biteko amesema kuwa lengo la Serikali ni kuwa na mtandao mkubwa wa mabomba ya gesi  pamoja na vituo vya kujazia gesi kwenye magari ili kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi.

Kutokana na hilo Dkt.Biteko ameeleza kuwa Serikali ipo tayari wakati wowote kutoa ushirikiano kwa kampuni zinazotaka kuwekeza kwenye kutoa huduma hiyo kwa wananchi.

Kwa upande wake, Farhiya Warsame amemshukuru Dk.Biteko kwa miongozo yake ambayo imepelekea kampuni hiyo kuanza kutekeleza mradi huo.

Ameeleza kuwa wananchi wameonesha mwamko mkubwa kwenye kuendesha vyombo vyao vya usafiri kwa kutumia gesi asilia badala ya mafuta kutokana na gesi asilia kuwa na gharama nafuu kuliko mafuta.

Vilevile, Dk. Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa kampuni ya Rock Mountain ya nchini Canada, Bw. Nick Lenstra ambayo imesaini Mkataba wa Ushirikiano na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa ajili ya kuanza kazi za upembuzi yakinifu na kuzungumza na wadau wa ndani ikiwemo Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) ili kutumia gesi asilia kutengeneza nishati kwa njia ya kimiminika ambayo inaweza kutumika kwenye ndege. 

Hali kadhalika, Dk.Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa kampuni ya CNOOC kwa upande wa Uganda, Wang Juteng ambapo pamoja kuzungumzia Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia nchini, ameikaribisha kushiriki Duru ya Tano ya Kunadi Vitalu vya Mafuta na Gesi Asilia nchini.