WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuongoza matembezi ya hisani yatakayoratibiwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kesho yakiwa na lengo la kuhamasisha jitihada za serikali kuelekea kufanikisha mpango wa kuwezesha kila mwanafunzi kuwa na kitabu kimoja.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa TET Dk. Aneth Komba, matembezi hayo yatakayofanyika kesho Ijumaa Machi 7, mwaka huu yatakuwa na kaulimbiu isemayo (Tembea na mheshimiwa kuunga mkono juhudi za serikali za kuhakikisha kila mtoto anakuwa na kitabu kimoja).
Amesema fedha itakayopatikana katika matembezi hayo yote itaenda kutengeneza kitabu kwaajili ya wanafunzi, akieleza kuwa kwa wale watakao penda kuunga mkono juhudi hizo kwa kushiriki wanaweza kununua sare ambayo ni Flana Sh. 50,000 na Traki Suti 150,000 kupitia namba ya serikali ya malipo ambayo ni 994040118259.
“Kila kitabu kimoja kinathamani kati ya 2,000 hadi 2,500 na kwa kweli tumedhamiria tukusanye hizi fedha tuchape vitabu ili kuwezesha kila mwananfunzi kuwa na chakwake.
“Pia tunafahamu kuwa kuna ukuaji mkubwa wa sayansi na teknolojia na sera yetu inasisitiza sana matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji, hivyo katika fedha zitakazopatikana tutatenga kiasi kitakachokwenda kununua kompyuta kwaajili ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita,” amesema Dk. Aneth.
Ameongeza kuwa watashirikiana na wadau ili wanafunzi wa kidato cha tano na sita badala ya kupatiwa kitabu wao wapatiwe kompyuta kila mpja yakwake ikiwa na kila kitabu, na maktaba mtandao.
Pia amebainisha kuwa wanataraji kwenda kwenye mikoa takribani 10 ili wanafunzi hao kila mmoja awe na kompyta yake.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED