RCC Mara yapendekeza jimbo la Serengeti kugawanywa

By Ambrose Wantaigwa , Nipashe
Published at 06:55 PM Mar 06 2025
Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi akiongoza kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa Mara(RCC)katika ukumbi wa uwekezaji mjini Musoma,kushoto ni Katibu Tawala Msaidizi (Mipango na Uratibu)Emmanuel Mazengo.
PICHA:MPIGAPICHA WETU
Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi akiongoza kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa Mara(RCC)katika ukumbi wa uwekezaji mjini Musoma,kushoto ni Katibu Tawala Msaidizi (Mipango na Uratibu)Emmanuel Mazengo.

Wajumbe wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mara (RCC) wamepitisha Jimbo la Uchaguzi la Serengeti kugawanywa na kupata majimbo mawili ya uchaguzi ambapo majina ya majimbo yanayopendekezwa ni Serengeti Mashariki na Serengeti Magharibi.

Mkuu wa Mkoa wa Mara Evans Mtambi aliongoza kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji ambapo aliwataka wakurugenzi wa Halmashauri kujiandaa kuweka mikakati ya ukusanyaji wa mapato ili kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi.

Hatua hiyo inakuja wakati tayari Tume huru ya taifa ya uchaguzi(INEC) imetangaza mchakato wa kupokea mapendekezo ya kugawa majimbo zoezi linaloendelea kuanzia Februari 27 na litakamilika Machi 26 mwaka huu.

Kulingana na tangazo la Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya uchaguzi INEC, Jaji Jacobs Mwambegele Tanzania ina jumla ya majimbo ya uchaguzi 264 ambapo Bara kuna jumla ya majimbo 214 na visiwani Zanzibar yakiwa 50

Mtambi amezitaka Halmashauri zote 9 mkoani humo kuongeza juhudi katika makusanyo ili kusogeza huduma za jamii karibu na wananchi kama maandalizi ya kuhudumia maeneo mapya ya uwakilishi ikiwa yatakubaliwa.

Baadhi ya wabunge kutoka mkoa wa Mara walishangazwa na namna Halmashauri kadhaa zilishindwa kutumia fedha zilizotengwa zaidi ya 14b/- kutekeleza miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Mbunge wa Tarime vijijini, Mwita Waitara alisema hatua hiyo haitendi haki kwa wananchi wa kawaida ambao wana uhitaji wa huduma kama vile afya,elimu, miundombinu na maji.

Akiwasilisha mpango wa bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2023/2026 Katibu Tawala Msaidizi(mipango na Uratibu)Emmanuel Mazengo amesema mwaka 2025/2026 Mkoa wa Mara unatarajia kukusanya mapato ya ndani yanayokadiriwa kufikia 47,194,453,000.

Vipaumbele vya bajeti ya Mkoa wa Mara kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 ni uboreshaji wa sekta ya elimu, huduma za afya, huduma za utawala na kuweka mazingira wezeshi na kuboresha usimamizi wa uchumi na uzalishaji. 

Miradi inayotegemewa kutekelezwa ni pamoja na ukamilishaji wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama, ujenzi wa nyumba ya kupumzikia viongozi, ununuzi wa gari, ukarabati wa nyumba ya Mkuu wa Mkoa na usimamizi wa mitihani.