Waziri Ndejembi aitaka TANESCO kusambaza Mita Janja nchi nzima

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:13 PM Dec 05 2025
Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi.

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amelielekeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha linasambaza mita janja mpya za umeme katika mikoa yote nchini ili kuongeza ufanisi, kurahisisha huduma kwa wateja na kuendana na maendeleo ya teknolojia.

Ndejembi ametoa agizo hilo leo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa mita janja hizo kwa wateja wa TANESCO, akisisitiza kuwa mifumo ya mita hiyo lazima iboreshwe kila mwaka ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia na mahitaji ya sasa.

Aidha, Waziri Ndejembi ametaka TANESCO kuhakikisha wateja wapya wanaotaka kuwekewa mita janja wanahudumiwa haraka, sambamba na kuwa na huduma kupitia aplikesheni maalumu itakayowezesha wateja kufuatilia mwenendo wa matumizi yao ya umeme kwa urahisi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema mita janja hizo zina faida nyingi ikiwemo uwezo wa kutunza kumbukumbu kwa muda mrefu na kutoa suluhisho endapo mteja atanunua umeme kwa bahati mbaya au kukosea taarifa.

“Zinabeba taarifa zote muhimu kuhusu mwenendo wa matumizi ya umeme, hivyo zitapunguza mawasiliano ya mara kwa mara kati ya shirika na wateja. Pia zina mifumo madhubuti ya kiusalama na kulinda uthibiti wa mapato,” amesema Twange.

Uzinduzi wa mita janja unatajwa kuwa hatua muhimu katika mageuzi ya digitali ndani ya sekta ya nishati, ikilenga kuongeza uwazi, ufanisi na kupunguza changamoto za muda mrefu katika usambazaji na udhibiti wa umeme nchini.