WHO yaitambua Novemba 17 Siku ya Watoto Njiti Duniani

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 11:32 AM May 30 2025
WHO yaitambua Novemba 17 Siku ya Watoto Njiti Duniani
Picha: Mtandao
WHO yaitambua Novemba 17 Siku ya Watoto Njiti Duniani

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza rasmi kuijumuisha tarehe 17 Novemba katika kalenda yake ya kimataifa kama Siku ya Watoto Njiti Duniani, ikiwa ni hatua muhimu ya kutambua na kuhamasisha jitihada za kulinda maisha ya watoto wanaozaliwa kabla ya muda kamili wa ujauzito.

Hatua hii ni ushindi mkubwa kwa sekta ya afya ya uzazi duniani, na hasa kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania, ambazo zimekuwa mstari wa mbele katika kupigania uboreshaji wa huduma kwa watoto wachanga, hususan wale njiti. WHO imesisitiza kuwa kuwepo kwa siku hiyo kutasaidia kuongeza uelewa, kuimarisha sera za afya na kuvutia uwekezaji zaidi katika huduma za watoto wachanga.

Tanzania yaandika historia kupitia juhudi za Doris Mollel

Tanzania imechukua nafasi ya kipekee katika mafanikio hayo kupitia juhudi za muda mrefu za Doris Mollel, mwanzilishi wa Doris Mollel Foundation (DMF). Doris, ambaye alizaliwa njiti, amegeuza simulizi yake kuwa chachu ya mabadiliko kwa watoto wengine waliopitia changamoto kama alizopitia yeye.

Kwa zaidi ya miaka saba, taasisi yake imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya kutoa elimu kwa jamii kuhusu watoto njiti, kuchangisha na kusambaza vifaa tiba kwa hospitali nchini, na kuwajengea uwezo wahudumu wa afya wanaohudumia watoto hao. Zaidi ya hospitali 20 zimepata msaada wa incubator, mashine za oksijeni, vifaa vya kupima joto, na usaidizi wa mafunzo kwa wauguzi kupitia DMF.

Akizungumzia uamuzi huo wa WHO, Doris amesema:

"Kupitishwa kwa Novemba 17 na WHO ni heshima kubwa kwa watoto njiti duniani. Kwa upande wangu binafsi na kwa Tanzania, hii ni zawadi ya juhudi za miaka mingi. Ninaamini sasa dunia itasikia kilio cha watoto hawa na kuchukua hatua madhubuti.


"What a Proud Moment! Ahsante sana Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Rais Dr @samia_suluhu_hassan huu ni ushindi mwingine wa ushawishi kutoka Tanzania.
Nashukuru sana @wizara_afyatz pamoja na @wizara_mambo_ya_nje_tz kwa kufanya kazi nasi kwenye hili muhimu kwa Taifa na Dunia kiujumla. @dorismollelfoundation ilikutana na @drtedros kujadiliana nae juu ya Siku hii muhimu na hili ni moja kati ya matokeo mazuri ya kazi yetu. Huu ni Mfano Mzuri wa namna Serikali yetu inafanya kazi na Mashirika yasio ya kiserikali.


Kipekee nakushukuru sana Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani @who @drtedros kwa uongozi na support kubwa uliyotupa wewe pamoja na ofisi yako, Ubalozi wetu Geneva @ubalozigeneva Mhe Balozi @hoycetemu


Ahsante nchi wanachama wote kwa kuunga mkono na kubariki Siku hii iwepo kwenye Kalenda ya Shirika la Afya Duniani, naamini uwepo wa siku hii na kutambulika kimataifa utazidi kuongeza chachu ya maboresho ya huduma za afya kwa Mama na Mtoto pamoja na vijana. Nina Tarajia tutafanya kazi kubwa ya kuhamasisha mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa ujauzito ili kupunguza watoto Njiti kuzaliwa lakini pia hata wakizaliwa kuendelea kuboresha huduma za watoto wachanga Duniani.

I am proud !

Serikali ya Tanzania yapongezwa kwa ushirikiano na dhamira ya dhati

Mbali na jitihada za DMF, Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya imetajwa kuwa miongoni mwa wadau waliounga mkono mchakato wa kuidhinisha siku hiyo. Serikali imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ya kupunguza vifo vya watoto wachanga kwa kuboresha huduma za afya ya uzazi, kujenga vitengo maalum kwa watoto njiti katika hospitali za umma na kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Afya, Tanzania imeongeza idadi ya vitengo vya kuhudumia watoto njiti katika hospitali za mikoa na wilaya, sambamba na kusambaza vifaa tiba vya msingi vinavyohitajika katika huduma hizo.

Msemaji wa Wizara hiyo amesema:

"Tunatambua umuhimu wa kuwalinda watoto wachanga, hususan wale njiti. Ushirikiano wetu na wadau kama Doris Mollel Foundation umesaidia sana kuongeza uelewa, kupunguza unyanyapaa na kuimarisha huduma hizi katika maeneo mengi ya nchi."

Takwimu zasema yote – na changamoto bado zipo

Kwa mujibu wa WHO, kila mwaka zaidi ya watoto milioni 15 huzaliwa njiti duniani, na kati yao, takriban milioni moja hufariki dunia kutokana na matatizo yanayohusiana na kuzaliwa kabla ya wakati. Afrika, ikiwemo Tanzania, inaongoza kwa idadi ya watoto njiti huku ikikumbwa na changamoto ya upungufu wa vifaa tiba, rasilimali watu na elimu ya jamii kuhusu mahitaji ya watoto hao.

Hata hivyo, hatua ya WHO kuutambua rasmi Novemba 17 kama siku maalum inaonekana kama fursa adhimu ya kuongeza ushirikiano wa kimataifa, kushirikisha sekta binafsi, na kuhakikisha kuwa kila mtoto anapewa nafasi ya kuishi na kufikia ndoto zake.