VIONGOZI mbalimbali wa Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) waliofika nyumbani kwa Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama, eneo la Itega jijini Dodoma, kutoa salamu za pole kufuatia kifo chake kilichotokea ghafla asubuhi ya leo, wameeleza ya moyoni kuhusu kiongozi huyo.
Akizungumza mara baada ya kusaini kitabu cha maombolezo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe, amesema taifa limepoteza kiongozi aliyekuwa mwema, mchapakazi na mzalendo.
“Ni msiba mkubwa kwa nchi. Mhagama alikuwa mtu wa upendo, aliyeacha alama kubwa katika jamii na kufanya kazi kwa ushirikiano. Atakumbukwa kwa uchapa kazi wake na uadilifu,” amesema Prof. Shemdoe.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema marehemu alikuwa Mbunge kwa miaka mingi na alitoa mchango mkubwa katika maendeleo ya mkoa huo, ikiwemo uendelezaji wa Jiji la Dodoma.
“Ameutumikia mkoa na taifa kwa moyo wa upendo. Dodoma imeguswa na mengi aliyoyafanya, na mchango wake utaendelea kukumbukwa,” amesema Senyamule.
Awali, Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, alitoa taarifa rasmi kwa vyombo vya habari akithibitisha kifo hicho. Marehemu Mhagama amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi serikalini, zikiwemo Naibu Waziri na Waziri kamili katika wizara tofauti.
Kabla ya kuanza kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, alikuwa Waziri wa Afya. Kwa sasa, Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na familia inaendelea kuratibu mipango ya mazishi, na taarifa zaidi zitatolewa kadri maandalizi yatakavyokamilika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED