Ajali za ndege zilivyotikisa, kuua vigogo Afrika, M/Kati

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 11:00 AM Dec 18 2024
Ajali ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Kenya, Francis Ogolla
Picha: Mtandao
Ajali ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Kenya, Francis Ogolla

WAKATI 2024 ukibakiza wiki chache kumalizika, yako matukio ambayo yameacha kumbukumbu kwenye uwanja wa kimataifa kama vile ajali na vita.

Ajali za ndege zimeua viongozi Afrika pamoja na Mashariki ya Kati mataifa ya Palestina na Iran.

Juni mwaka huu, inasikika ajali ya ndege, ikimaliza maisha ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa Malawi, Dk. Saulos Chilima.

Ajali hiyo ilisababisha kifo chake na  abiria wengine huku ikiacha simanzi kwa familia, wafuasi na Wamalawi.

Chilima na maofisa wengine alikuwa akisafiri kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa waziri wa serikali hiyo, Ralph Kasambara.

Mke wa rais wa zamani Bakili Muluzi, Shanil Dzimbiri ni miongoni mwa abiria waliokuwa kwenye ndege hiyo.

Ndege aina ya Dornier 228 ilitangazwa  kupotea kwenye rada ilipofikia eneo la hifadhi ya misitu Chikangawa na Juni 11, mwaka huu, ikathibitishwa imepata ajali.

Chilima, alikuwa mwanasiasa maarufu katika siasa za Malawi, na kabla ya kujiunga na siasa alichangia kukua kwa kampuni ya Airtel nchini humo na kukuza mapato.

Kisiasa, alihudumu katika kiti hicho tangu mwaka 2014 akipambana na rushwa na kukumbana na changamoto kadhaa. Mazishi ya kitaifa yaliangazia mchango wake katika nchi.

Chilima alikuwa amerejea muda mfupi  kutoka katika ziara ya kikazi nchini Korea Kusini, kwenye kongamano la Korea Afrika Summit, jijini Seoul. 

Kabla ya kifo cha Chilima, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Kenya, Francis Ogolla, anaangamia kwenye ajali ya ndege, Mei mwaka huu.

Ulikuwa mwaka wa ajali za anga ambayo pia ilikatisha uhai wa Rais wa Iran, Ebrahim Raisi, yote yakiacha simanzi kwa mataifa wafiwa.

KILIO KENYA

Aprili, mwaka huu, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Kenya, Francis Ogolla alifariki kwa ajali ya helikopta.

Rais wa Kenya, William Ruto anatangaza kifo cha Ogolla pamoja na maofisa wengine tisa wa jeshi, huku wawili wakinusurika.

Ogolla anafariki baada ya helikopta aliyokuwa akisafiria pamoja na maofisa wengine kuanguka eneo la Kaben, Marakwet.

Ogolla alichukua nafasi ya kuongoza jeshi tangu Aprili 28, mwaka 2023.

Mashuhuda wanasema ndege ilishika moto wakati wa kuanguka. Eneo hilo lilizingirwa baada ya ajali hiyo.

Maofisa hao walikuwa wakichunguza eneo hilo, kabla ya kutumwa kwa wanajeshi zaidi kukabiliana na wezi wa mifugo.

Helikopta hiyo ya Jeshi la Anga la Kenya aina ya Huey, ilikuwa imetoka katika shule moja ya msingi kabla ya kuanguka na kuwaka moto.

Ogolla, alichukua uongozi wa jeshi kutoka kwa Jenerali Robert Kibochi, baada ya kufikisha umri wa kustaafu.

SIMANZI IRAN

Mei, mwaka huu, Rais wa Iran, Ebrahim Raisi, pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje, Hossein Amir-Abdollahian na wengine saba, walifariki dunia katika ajali ya helikopta iliyotokea kaskazini-magharibi mwa Iran.

Shirika la Habari la Serikali (IRNAA), linasema ndani ya ndege hiyo pia alikuwamo Ayatollah Mohammad Ali Al-e Hashem, imamu wa Swala ya Ijumaa katika mji wa Tabriz na Jenerali Malek Rahmati, Gavana wa Jimbo la Iran la Azabajani Mashariki.

Kamanda wa Kitengo cha Ulinzi wa Rais, Sardar Seyed Mehdi Mousavi, pia aliuawa, pamoja na walinzi kadhaa na wafanyakazi wa helikopta ambao bado hawaja tajwa.

MAUAJI HAMAS 

Wanajeshi wa Israel walikuwa wanamwinda kwa zaidi ya mwaka mmoja kiongozi wa Hamas, ambaye alitoweka huko Gaza mara tu baada ya kupanga mashambulizi ya Oktoba 7, mwaka 2023.

Yahya Sinwar (61), inasemekana alitumia muda wake mwingi kujificha kwenye vichuguu chini ya ukanda huo, pamoja na kada ya walinzi na ya mateka waliokamatwa kutoka Israel.

Jeshi la Ulinzi la Israel, linasema kuwa kikosi cha 828 cha Biislamach Brigade kilikuwa kikishika doria Tal al-Sultan, eneo la Rafah.

Lakini hatimaye, alikutana na mwisho wake katika kukutana na doria ya Israel kusini mwa Gaza, alikuwa na idadi ndogo ya walinzi. Hakuna mateka waliopatikana.

Wanamgambo watatu walitambuliwa na walipambana na wanajeshi wa Israel na wote waliuawa.

Kifo cha Sinwar ni pigo kubwa kwa Hamas, lakini haukuwa mwisho wa vita.

Mwili ulitolewa na kupelekwa Israel, baadaye eneo hilo liliwekwa salama.

Daniel Hagari, msemaji wa IDF, alisema vikosi vyake "havikujua kuwa alikuwa huko lakini tuliendelea kufanya kazi, alikimbia peke yake kwenye moja ya majengo na aliuawa baada ya kupatwa na ndege isiyo na rubani.”

MILIPUKO YA SIMU

Tukio lingine kwa mwaka huu, ni vifo vya takribani watu 26 wakiwamo watoto wawili, waliuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa.

Wengi wao wakiwa vibaya, baada ya vifaa vya mawasiliano vingine vinavyotumiwa na kundi lenye silaha la Hezbollah, kulipuka kwa kiasi kikubwa kote nchini Lebanon.

Katika tukio la milipuko, ilijeruhi takribani watu 450, kulingana na Wizara ya Afya ya Lebanon.

Milipuko hiyo ilitokea karibu na umati mkubwa wa watu waliokuwa wamekusanyika, kwa ajili ya mazishi ya wahanga wanne wa milipuko hiyo ya Jumanne.

Milipuko hiyo ilizidisha hali ya wasiwasi katika jamii ya Lebanon, ikitokea siku moja baada ya shambulio kama hilo.

Makampuni mawili yaliyoko Taiwan na Hungary yanayoshutumiwa katika ripoti za vyombo vya habari kwa kutengeneza vifaa hivyo na nchi zote hizo zilikana kuhusika.

KUONDOSHWA ASSAD

Rais wa Syria, hivi karibuni na serikali yake ameng’olewa madarakani. Bashar al-Assad, alitolewa kimabavu baada ya kundi la waasi kuongoza maasi dhidi yao Jumapili, Desemba 8, 2024.

Familia ya Assad imeitawala Syria kwa miaka 53, Assad alichukua madaraka mwaka 2000, baada ya babake kutawala kwa miaka 30.

Miaka 13 iliyopita, anatumia nguvu kuwakandamiza waandamanaji na kisha kukawa na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Zaidi ya watu 500,000 wameuawa na wengine milioni 12 wamelazimika kukimbia makazi yao.

Lakini Jumatano wiki iliyopita, kundi la Kiislamu, Hayat Tahrir al-Sham (HTS), lilifanikiwa kufanya mashambulizi mabaya kaskazini magharibi mwa nchi hiyo, baada ya kushirikiana na makundi mengine ya waasi.

Waasi hao waliuteka mji wa pili kwa ukubwa nchini Syria, Aleppo na kuelekea kusini hadi mji mkuu, Damascus, ambako walizidi nguvu jeshi la Syria.

Russia, baadaye ilitangaza kuwa Assad na familia yake wamepewa hifadhi ya kisiasa huko Moscow.

MOTO GAZA 

Tangu kuanza kwa vita huko Ukanda wa Gaza, idadi ya vifo imefikia watu 45,000 kwa mujibu wa kituo cha Aljazeera.

Sasa vita hiyo inatimu miezi 15 ni kati ya matukio ya kimataifa ambayo yamekuwa yakiwaumiza vichwa wapatanishi wa kimataifa.

Katika idadi hiyo ya vifo wamo watoto 17,000 achilia mbali watu 11,000 ambao wameripotiwa kutoweka wakihofiwa wamefukiwa na vifusi.

BBC/ALJAZEERA