Mafundi cherehani walivyo kundi muhimu, wakifunguka kiuchumi daima hawasogei

By Christina Haule , Nipashe
Published at 08:07 AM Apr 05 2024
Baadhi ya mafundi Cherahani katika ofisi ya pamoja, eneo la Dumila, wilayani Kilosa wakishona nguo.
Picha: Christina Haule
Baadhi ya mafundi Cherahani katika ofisi ya pamoja, eneo la Dumila, wilayani Kilosa wakishona nguo.

HUDUMA ZA mafundi cherehani ni kongwe na ziko kila mahali nchini. Ila wenyewe wanalalamikia katika manufaa ya huduma hiyo, hawanufaiki na nyenzo za kiuchumi zinazowakweza.

Sasa wako katika maombi ya kusaidi kushona nguo wanapata mikopo itakayowasaidia, mitaji na ununuzi wa mashine za kisasa, hata ikarahisisha utoaji huduma kwa wateja, huku wakiongeza kipato kwa maendeleo yao na taifa.

Mwalimu wa Cherahani na Ushonaji Nguo kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda vidogo (SIDO) mkoani hapa, Isack Maufi, anasema mafundi wengi wa nguo wako chini kiuchumi.

Anafafanua wanaishi katika nyumba za kupanag, hawana magari na hawadhamiki kwa mikopo wanayoihitaji.

“Unapozungumzia suala la mitaji, bado gumu kwa mafundi nguo, kwa  sababu hatuna thamani inayohamishika na kutuwezesha kupata mikopo,” anasema Maufi.

Akirejea uzoefu wake wa miaka 20 kwenye ufundi cherehani na kushona, bado hajafanikiwa kufikia miliki hizo, kikuu wanaishia kujikimu na kisaiodai ndugu wa karibu.

Fundi huyo anasema, wakiwa na mashine za kusukuma kwa mguu kila siku, huwaondolea kujiamini, hawavutiwi na kazi zao, pia hawawezi kufanikiwa, bali mashine za umeme ndizo zinawawezesha kuendelea.

Katika hilo, anwaasa mafundi wenzake kujiunga katika vikundi hata inakapotokea nafasi wao kukopeshwa mitaji mikubwa, inakuwa rahisi wakainuka kiuchumi na kuboresha maendeleo, kama mafundi wengine aina yao wanavyoinuka.

Anaeleza wakipata mitaji mikubwa itawawezesha kununua vifaa vya kisasa, majora ya vitambaa, kufungua au kukodi fremu za biashara, kushona nguo na watakazoziuza kwenye magulio na masoko makubwa, wakajiongezea kipato.

“Mshonaji anaweza kuwa na mawazo makubwa kwamba anunue mashine ya umeme ambayo ni rahisi, lakini suala la mtaji ndio humfanya kubaki akitumia mashine za kusukuma na miguu, ambayo humchukua muda mrefu kukamilisha kushona nguo moja, tofauti na akiwa na mashine ya kisasa ya umeme ambayo humuwezesha kushona hata nguo tatu kwa siku” anasema Maufi.

Pia, anataja mikopo mikubwa kwa mafundi kushona ina nafasi kuinua taaluma ya ushonaji nguo, hata kuwafanya mafundi chipukizi kuziona chachu za kazi yao.

Anasema, kazi inapokuwa nzuri inapaswa kukimbiliwa hata na vijana, katika nyakati zilizopo kukabiliana na wimbi wa ukosefu wa ajira nchini.

Maufi anasema, vijana wanaoanza kazi wakitoka mafunzoni, ni kundi ambalo likipatiwa mikopo, wanamudu kukwea kujiongezea ujuzi, katika uandaaji bidhaa za kufikia sokoni.

“Fundi chipukizi wa sasa anapaswa kukua kila siku na kutokuwa fundi chipukizi wa kizamani, ambaye alibaki kila siku kutoa mashine yake moja nje kwenye kibaraza chao ambayo wakati mwingine haina hata nyuzi za kushonea. 

“Hali hii huwafanya mafundi chipukizi wengi kukata tamaa na kujiunga kufanya kazi viwandani, wakiamini watapata fedha nyingi tofauti na walipo,” anatamka.

AIPONGEZA SIDO 

Maufi anaipongeza SIDO kwa kuona umuhimu wa kutoa elimu ya ushonaji wanafunzi 34 wa kike, akimini wanapokamilisha mafunzo hayo ya miezi mitatu, wanakuwa nafasi kubwa ya kujikita kwenye soko la ushonaji.

Pia, Maufi anatumia fusra hiyo tajwa, akiiomba serikali ishiriki katika uingizaji mashine za chereheni umeme nchini, zenye gharama nafuu, tofauti na zilizopo sokoni sasa.

“Cherahani ya umeme moja ikiingia nchini huuzwa hadi shilingi laki saba hadi shilingi milioni moja,” anasema Maufi.

Vilevile, anaiomba serikali kuangalia suala la kuboresha na kuimarisha upatikanaji umeme, ili kuwezesha uhakiki wake, ikifanikisha maendeleo ya viwanda nchini. 

DARASA ALIYEFANIKIWA 

Rehema Sambui, mwanamke aliyefanikiwa katika ushonaji nguo, akitokea Kata ya Dumila wilayani Kilosa mkoani hapa, anaishukuru SIDO kuwapa mafunzo ya ushonaji wao watu 20, ikiwapatia cherahani kila mmoja.

Anasema baada ya kupata cherahani hiyo, mwaka 2021 wakafungua ofisi zao na wakaunda kikundi walichokiita ‘Tujitume’ chenye watu 18.

Rehema anaeleza, wakafungua ofisi tatu, ikiwamo ya kushona mabegi ya mapambo na kushona nguo za kawaida za maharusi.

Katika ufafanuzi wake, anasema nje ya kikundi ana ofisi binafsi yenye mashine nane, huku akiwa na vijana aliowaajiri zaidi ya 10,  anaowalipa kila mwezi kwa mapatano tofauti.

Anasema ufundi unamsaidia kuendesha familia yake huku akiwa na mtoto mmoja na wazazi wake na wadogo zake ambao wanamtegemea.

Hata hivyo kuhusu masoko, mama huyo ana ufafanuzi kwamba, SIDO imewasaidia mafunzo cherahani na elimu ya masoko, hivyo imewawezesha kuomba na kupata tenda kupitia kwenye shule za serikali na watu binafsi.

Kwa mujibu wa Mama Rehema, ni hali inayowainua kiuchumi, ikiendana na mabadiliko ya mtaji kiuchumi, ikilingainishwa na nyuma walipoanza ufundi.

MENEJA SIDO

 Hadi sasa, Meneja wa SIDO mkoa wa Morogoro, Joan Nangawe, anasema shirika lake linasambaza teknolojia ya msingi, mafunzo na kuwezesha wajasiriamali kupata masoko na mitaji, huku wakianzisha kituo maalum cha mafunzo na ubunifu kuwasaidia vijana.

Anasema kuanzishwa kwa kituo kumesaidia kuwawezesha wajasiriamali wanaochipukia kupata huduma ya teknolojia, ikiwamo mashine ndogo wahusika wakipewa mafunzo na zinatumika kama vitendea kazi.

Meneja Nangawe anasema, wameanzisha huduma ya kujifunza ujuzi wa kutengeneza vyerehani na kufundisha ushonaji nguo, ili kuwawezesha wahitaji  kuzalisha vitu vitakavyokidhi mahitaji ya soko.

Kukitajwa sasa wameshaanza na wanafunzi 34 wakaotapewa cherehani za ruzuku kila mmoja watakapomaliza mafunzo, yatakayodumu kwa kipindi cha miezi mitatu.

Nangawe anaeleza mategemeo ni kuyaona matokeo mazuri kwa wanafunzi, baada ya mafunzo kukamilika, ili kuimarika kiujuzi na kukabiliana na changamoto za kimaisha ikiwamo ukosefu wa ajira.

Anarejea kwamba kituo hicho kimeanzishwa tangu mwaka 2023, kikishirikiana na SIDO Mkoa Mwanza kukiwapo wanafunzi 20 kutoka eneo la Dumila, Kilosa, waliofundishwa.

Baada ya hapo, wakakabidhiwa cherahani za ruzuku za shilingi milioni mbili, kuwezesha ushonaji kisasa na wenye manufaa kiuchumi.

Nagawe anasema, wanatazamia kila robo ya mwaka wawe na wanafunzi 30, hata mwisho wa mwaka wawe wamewaelimisha vijana 120 katika fani mbalimbali za ushonaji.

Hapo anataja ushonaji mavazi ya kike, kiume na zingine kama sherehe, mapambo ya nyumbani vitambaa na mashuka, wanaofunzwa kuvshwa kutoka hatua moja hadi  nyingine, bila ya gharama kimitaji.

Hivyo, anawataka vijana wasibweteke kukaa nyumbani, bali wahakikishe wanapata mafunzo ya fani ili kuimarisha ujasiriamali wao.